WIKI moja imekatika tangu rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma ajisalimishe polisi na kukabidhiwa mikononi mwa mamlaka ya magereza kwenda kutumikia kifungo cha miezi 15.

Awali rais huyo mstaafu alipinga hukumu ya miezi 15 ambayo ilitolewa na mahakama kuu nchini Afrika Kusini kwa kosa la kudharau amri ya mahakama kwa kutoitikia wito wa kwenda kusikilizwa kesi za rushwa na zinazomkabili.

Zuma pia aliilalamikia huku hiyo akisema sio ya haki kwa upande wake, akalalamikia afya yake kwamba hastahili kukaa jela, lakini mwishowe alikubali kufuata sheria na kujisalimisha kwa hiyari yake kwa mamlaka nchini humo.

Zuma aliwaambia maelfu ya wafuasi wake waliokuwa wamekusanyika nje ya makaazi yake ya Nkandla kuwa alinyimwa haki zake za kikatiba na majaji wa mahakama ya katiba nchini humo.

“Siombi kuonewa huruma lakini nataka haki. Umri wangu na hali yangu ya kiafya pamoja na mambo mengine hayakuzingatiwa wakati uamuzi ulipotolewa”, alisema.

Zuma, aliwaongoza wafuasi wake kuimba wimbo maarufu wakati wa enzi za kupambana na ubaguzi wa rangi wa “Umshini Wami” ukimaanisha niletee bunduki yangu, wimbo ambao amekuwa akiitumia sana katika mikutano yake ya siasa.

Kabla ya kufikia uamuzi kwa Zuma kujisalimisha polisi na hatimaye kupelekwa jela, wafuasi wake walizingira nyumba yake wakipinga kukamatwa kwa rais huyo mstaafu ambaye ni kipenzi chao.

Wafuasi hao walisema wako tayari kumlinda Zuma kwa gharama yoyote ikiwezekana wapo tayari kupambana na polisi ili kuzuia zoezi la polisi kutumia nguvu kukamatwa kwa Zuma.

“Tuko hapa kumlinda Zuma asikamatwe. Yeyote anayetaka kumkamata lazima atukamate sisi kwanza, ndio maana tuko hapa. Wakija hapa kesho, tukawepo hapa hapa. Hata kama itachukua mwaka mzima, watatukuta hapa. Tutazuia mtu yeyote atakayejaribu kumkamata msholozi mbele yetu”.

Hata hivyo ikiwa wiki moja imepita tangu Zuma akibali kwa hiyari yake kujisalimisha jela wafusi wake wameingia mitaani wakifanya maandamano wakitaka kiongozi wao huo atolewe jela.

Maandamano hayo yamegeuka kuwa vurugu na kusabisha uporaji kiasi cha vikosi vya usalama kujitosa kukabiliana na machafuko hayo yanayohatarisha usalama wa nchi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka nchini Afrika Kusini ghasia za kupinga kufungwa kwa Zuma zimesababisha watu kadhaa kufariki huku wengine zaidi ya 200 wakiripotiwa kujeruhiwa.

Ghasia hizo awali zilitokea katika mkoa wa Kwazulu Natal anakotokea Zuma usiku wa siku ya kwanza wa Zupo alipoanza kutumikia kifungo chake cha miezi 15 gerezani.

Mbali na jimbo la KwaZulu-Natal, vurugu hizo zilienea hadi kwenye jimbo la Gauteng na jiji la Johannesburg. Waandamanaji walipora maduka, kuchoma moto majengo na magari na vilevile kuzuia barabara wakati wakiandamana kwenye miji hiyo.

Mjini, Eshowe, karibu na makaazi ya Nkandla ya Jacob Zuma, polisi walifyatua risasi mapema kuwatawanya waandamanaji waliopora na kuliteketeza duka kuu la mji huo.

Polisi nchini Afrika Kusini wanaeleza kuwa kuwa wahalifu wanatumia ghadhabu dhidi ya hatua ya kufungwa Zuma na kusababisha uharibifu wa mali, miundombinu na wizi.

Msemaji wa polisi Kanali Brenda Muridili amesema vifo hivyo vimetokana na ghasia na tayari uchunguzi unaendeshwa. Taarifa ya polisi imesema matukio ya garama na uharibifu wa mali yatatolewa baadaye.

Duka moja wapo la Durban liliporwa ambapo polisi walifyatua risasi ilikuwatawanya waandamanaji asubuhi ya leo kwenye mji wa Eshowe, karibu na makaazi ya Zuma ya Nkadla.

Akizungumzia ghasia hizo, rais Cyril Ramaphosa alisema machafuko yanavuruga juhudi za kuujenga uchumi wa nchi hiyo ambao umeathirika kwa kiasi kikibwa na janga la corona na kwamba hakuna uhalali wa kufanya vurugu wala uharibifu wa mali.

“’Tuwe wazi, kama taifa, kwamba hatutovumulia vitendo vyovyote vya uhalifu, hatutovumilia vitendo vyoyote vya uharibifu. Wale waliohusika na visa hivyo vya umwagikaji wa damu watakamatwa na kufunguliwa mashtaka”, alisema Ramaphosa.

Ramaphosa alisema ingawa kuna walioumizwa na wenye hasira kwa sasa kutokana na hukumu ya Zuma, nilazima wazingatie juhudi za kupambana na janga la corona nchini humo.

Ramaphosa alisema kwa kipindi cha wiki mbili, Afrika ya Kusini imeshuhudia visa 20,000 kwa siku vya maambukizi ya corona na watu 4,200 wamefariki mnamo kipindi hicho kutokana ugonjwa huo.

Kutokana na kuendelea kwa ghasia jeshi la Afrika Kusini limesema linapeleka wanajeshi katika majimbo mawili ilikukabiliana na ghasia zilizoibuka kufuatia kifungo cha Jacob Zuma.

Kabla ya tangazo la jeshi, vikosi vilionekana kwenye barabara za Pietermaritzburg, mji mkuu wa jimbo la KwaZulu-Natal, baada ya duka kuu kuchomwa moto hii leo Jumatatu. Benki, maduka na vituo vya kuuza mafuta vilifungwa katika mji huo.

Ghasia zimeendelea kuripotiwa katika wakati mahakama inajitayarisha kusikiliza pingamizi lililowasilishwa na upande wa Jacob Zuma dhidi ya kifungo cha jela.

Dali Mpofu wakili wa Zuma amewambia majaji tisa miongoni mwa 11 wa korti kuu kwamba hukumu iliotolewa dhidi ya mteja wake ilikuwa na makosa.

Alisema Zuma alihukumiwa kimakosa na hakutendewa haki katika upunguzwaji wa hukumu, lakini jaji Steven Majiedt alijibu akisema kuwa Zuma alihukumiwa kwa makosa ya kutoheshimu korti.

Licha ya kashfa za ufisadi zinazo mkabili, Zuma mwenye umri wa miaka 79, bado ni maarufu miongoni mwa wananchi wa Afrika Kusini hasa wale masikini sana.

Zuma alihukumiwa kifungo cha miezi 15 Jumanne wiki iliyopita baada ya kuudharau mara kadhaa wito wa mahakama wa kumtaka afike mbele ya tume maalum inayochunguza tuhuma za rushwa zinazo mkabili.

Zuma alikataa kufika mbele ya tume hiyo akitoa sababu kwamba Zondo anaupendelea upande mmoja na kuongoza uchunguzi huo kwa misingi ya kisiasa.