HIVI karibuni taifa changa barani Afrika liliadhimisha miaka 10 tangu lilipojipatia uhuru wake Julai 9 baada ya kutengana na Sudan Khartoum.

Wakati Sudan Kusini ilipojipatia uhuru wananchi walikuwa na matumaini makubwa ya kutimia kwa ndoto zao, hata hivyo baada ya miaka mitatu mafahali wawili rais wa nchi hiyo Salva Kiir na mpizani wake Riek Machar waliingia vitani.

Mzozo wao ulitokana na rais Kiir kumtuhumu Machar ambaye alikuwa makamu wake wa kwanza wa rais, kusuka mipango ya kumpindua na kumuondosha madarakani.

Mzozo huo ulisababisha vikosi vya serikali chini ya rais Kiir kupambana na wanajeshi waliokuwa wakimunga mkono Machar na hivyo kuzuka vita vya wenyewe kwa wenye.

Katika makala haya tutaangaliwa mafahali hawa wawili wametokea wapi? Tukianzia na Salva Kiir ambaye ni mpiganaji wa msituni aliyeongoza vya kupata uhuru miaka 10 iliyopita na kumaliza miaka zaidi ya 20 ya kupigania kujitawala kutoka kwa serikali ya Sudan.

Kiir ni muumini huyo wa dhehebu la kanisa katoliki, anafahamika sana kwa kutoa mahubiri katika kanisa kuu jijini Juba na anapenda sana kuvaa kofia nyeusi, aliyopewa zawadi kutoka kwa aliyekuwa rais wa zamani wa Marekani, George Bush.

Kiir aliyejaliwa urefu wa kimo na ndevu, alifahamika sana kwa kuongoza vikosi vya wapiganaji msituni, badala ya kutoa hotuba za kisiasa.

Alipigana msituni wakati wa vita vya kwanza vya Sudan vilivyoanza punde baada ya uhuru kutoka Uingereza kati ya mwaka 1956 hadi 1972, na baadaye kati ya 1983-2005, kudai uhuru wa nchi yake Sudan Kusini.

Hata hivyo, alichukua hatamu za uongozi la kundi lililokuwa linapigania uhuru wa nchi yake mwaka 2005 baada ya kifo cha kiongozi wake na mpiganaji wa siku nyingi John Garang, aliyefariki dunia kufuatia ajali ya helikopta.

Upinzani wake wa kisiasa na Makamu wake wa rais Riek Machar ulizua vita vipya katika taifa hilo changa duniani.

Tangu mwaka 2013 mapigano hayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 400,000 na visa vingine vya ukiukwaji wa haki za binadamu kama ubakaji wa wasichana na wanawake pamoja na mateso yakishuhudiwa.

Mzaliwa wa jimbo la Warrap mwaka 1951, kutoka kabila la dinka lenye watu wengi nchini Sudan Kusini, alitumia muda mrefu wa maisha yake akibeba bastola.

Punde tu, baada ya uhuru wa Sudan Kusini, taifa hilo chini ya Kiir, lilipata uungwaji mkono wa jumuiya ya kimaifa na kupata msaada wa mabilioni ya dola kuunga mkono miradi ya maendeleo.

Uongozi wake wa serikali baada ya miaka 10 ya uhuru, nchi hiyo imetawaliwa na ufisadi na mdororo wa uchumi.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa mwaka 2016 ilimshtumu yeye na Makamu wake Machar kwa kuhusika na machafuko yaliyoendelea kutokea nchini humo.

Aidha, Kiir ameripotiwa kujilimbikizia mali za umma na kuwekeza miradi binafsi ya kiuchumi kwa kiasi kikubwa nje ya nchi huku wananchi wake wakihaha kwa ugumu wa maisha, masikini, balaa la njaa na umasikini.

Shirika la kimataifa la utatuzi wa migogoro ICG linasema, rais Kiir abakia kuwa  kiongozi asiyetabirika, anayeongoza serikali isiyo imara na mpinzani wake Machar.

Anaelezwa kuwa mtu anayesikiliza zaidi kuliko kuongea na mara nyingi huwashangaza hata washauri wake kwa kubadilisha misimamo, wakati mwingine, anaelezwa kama kiongozi anayeweza kuliunganisha taifa lakini wakati mwingine, anayeweza kuligawa.

Fahali mwengine ni Riek Machar, kiongozi wa waasi mwenye historia nchini Sudan Kusini. Ni kiongozi wa kundi la waasi ambaye ndani ya miaka 10 sasa, amekuwa ndani na nje ya serikali.

Katika mzozo wa nchi hiyo, Machar anabakia kuwa kiungo muhimu, licha ya tabasamu lake la mara kwa mara, wanaomfahamu wanasema ana hasira na ni mkatili.

Alizaliwa mwaka 1953 katika jimbo la Unity. Kabila lake ni Nuer, jamii ya wafugaji nchini Sudan Kusini. Kabila lake ndilo la pili kwa watu wengi nchini Sudan Kusini baada ya lile la Dinka.

Hakupitia utamaduni ya kuchanjwa kwenye paja la uso, kuonesha utofauti ya wavulana na wanaume wa Nuer, lakini alipata nafasi ya kwenda skuli badala ya kuchunga mifugo.

Baada ya kusomea uhandisi katika chuo kikuu cha Khartoum, alipata shahada ya udaktari kutoka chuo kikuu cha Bradford nchini Uingereza.

Mwaka 1983, alirejea Sudan na kujiunga kwenye vita kati ya Sudan Kaskazini na Kusini na kupata uugwaji mkono wa Wanuer wenzake, waliomuamini anaweza kutoa uongozi kwenye kundi la waasi ambalo lilikuwa linaongozwa na wale kutoka kabila la Dinka.

Hata hivyo, alichukizwa na jaribio la kiongozi la kundi la waasi wakati huo John Garang, kujaribu kumundoa kama mmoja wa makamanda wa kundi hilo, yeyé pamoja na wenzake, akiwemo rais wa sasa Salva Kiir mwaka 1991.

Wakati kundi la waasi, lilipoendelea kugawanyika kwa misingi ya kikabila, Machar alishtumiwa kupanga mauaji dhidi ya waasi kutoka kabila la Dinka katika mji wa Bor mwaka 1991, katika mauaji ambayo yanasalia kuwa makubwa katika historia ya vita nchini humo.

Hii ilizua ulipizaji wa kisasi kati ya makundi ya makabila hayo mawili, yaliyokuwa yameoana na kushirikiana katika mambo mengi ya kijamii. Machar baadae aliondoa kwenye kundi kuu la waasi na kusaini mkataba na maadui wake wa zamani, serikali ya Khartoum.

Machar alirejea kwenye uwanja wa mapambano mwaka 2002. Baada ya mkataba wa amani kutiwa saini kati ya serikali ya Khartoum na waasi Kusini mwa nchi hiyo mwaka 2005, aliteuliwa kuwa makamu rais wa eneo la Sudan Kusini.

Hii ni nafasi aliyoendelea kuishika hata baada ya Sudan Kusini kupata uhuru wake mwaka 2011, huku Salva Kiir akiwa rais.

Baada ya kujitenga na Sudan, nchi hiyo mpya ilianza kushuhudia changamoto za kiuchumi. Wananchi wengi waliishi kwa taabu. Changamoto hizo, zilimsukuma atangaze kuwania urais mwaka 2015.

Hali hiyo ilisababisha sintofahamu katika serikali ya Kiir ambaye aliamua kumfuta kazi Machar na washirika wake, hali hiyo ilisababisha kuzuka vita na Machar akalazimika kuikimbilia Afrika Kusini na Ethiopia kwa nyakati tofauti.

Mwaka 2020, baada ya mkataba wa amani na rais Kiir mwaka 2018 aliapishwa kuwa Makamu wa rais kwa mara ya tatu. Machar amemwoa, Angelina Teny ambaye sasa ni waziri wa Ulinzi na wana watoto kadhaa.