MICHUANO ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Kombe la Kagame, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi rasmi Agosti 1-14 jijini Dar es Salaam.
Wawakilishi wa Zanzibar kwenye michuano hiyo, mabaharia wa KMKM wamepangwa kundi ‘B’ pamoja na KCCA FC (Uganda), Azam FC (Tanzania Bara) na Le Messager Ngozi (Burundi).
Kundi ‘A’ la michuano hiyo inayotarajiwa kuwa na ushindani linaundwa na Young Africans (Tanzania Bara), Nyasa Big Bullets (Malawi), Express FC (Uganda) na Atlabara FC (Sudan Kusini).
Tunachukua nafasi hii kuwatakia kila kheri wawakilishi wetu hao tukiamini wana kila sababu ya kufanya vizuri kutokana na maandalizi waliyofanya huku wakielewa jukumu kubwa walilolibeba mbele ya wananchi wa Zanzibari.
Michuano hiyo haijafanyika kwa miaka miwili kutokana na sababu ambazo zinaelezwa zilikuwa nje ya Baraza la Michezo Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ambalo ndiyo wasimamizi.
Kwa ujumla,Tanzania itakuwa na timu tatu baada ya Simba kujiondoa kwenye michuano hiyo kwa kile walichokieleza kutingwa na ratiba ya msimu mpya na ushiriki wa michuano ya CAF.
Kubwa tunalowakumbusha wawakilishi wetu hao kuhakikisha wanalinda heshima ya Tanzania kwa kulibakisha taji hilo kwenye ardhi yetu.
Ni ukweli usiopingika kuwa michuano hiyo ndiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, lakini, pia ikitambuliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na lile la Kimataifa (FIFA).
Haitopendeza ikiwa klabu zetu zitashindwa kubeba taji hilo ikizingatiwa namna zilivyofanikiwa kuweka historia hadi sasa ambapo Simba ndiyo kinara wake ikifuatiwa na Yanga na AFC Leopard.
Kwa mantiki hiyo, tuna kila sababu ya kuendelea na rekodi hiyo huku tukiamini zilifanya maandalizi ya kutosha sambamba na kubebwa na wachezaji wazuri kwenye ukanda huu.
Lakini pamoja na ukweli huo, pia tungelipenda kuzitahadharisha timu zetu kutojiamini sana ikizingatiwa wapinzani wetu nao wamejiandaa vya kutosha ili kuhakikisha wanalitwaa taji hilo.
Ukweli wa hilo ni kutokana na kiwango cha hali ya juu kilichoonyeshwa na watetezi wa michuano hiyo, KCCA iliyotwaa taji hilo miaka miwili iliyopita.Hivyo ni imani yetu kwamba wawakilishi wetu hao hawatarejea makosa hayo na badala yake kulibakisha Kombe la Kagame nyumbani kwa mara nyengine kama ambavyo ilishafanya hivyo huko nyuma.
Zanzibar Leo kama jamii ya wanamichezo tunazitakia kila la kheri klabu zetu zote tatu katika michuano hiyo, tukiamini tuna kila sababu ya kulibakisha kombe hilo nyumbani.