TOKYO, JAPANI

KIMBUNGA cha kitropiki cha Nepartak kinaelekea kaskazini magharibi juu ya bahari mashariki ya Japani na kutishia kukaribia au kufika mashariki mwa Japani au katika eneo la Tohoku leo.

Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa ya Japani inaonya kuwa kimbunga hicho huenda kikasababisha upepo mkali, mvua kubwa na mawimbi makubwa.

Mamlaka hiyo inasema Nepartak ilikuwa ikielekea kaskazini magharibi juu ya bahari na kuelekea mashariki ya Japani kwa kasi ya kilomita 35 kwa saa hadi kufikia jana mchana kwa saa za Japani.

Kina kitovu chenye mgandamizo wa angahewa wa hektopaskali 992 na upepo wa upeo wa juu wa kasi ya kilomita 72 kwa saa na dhoruba ya upeo wa juu wa kilomita 108 kwa saa.

Pepo za kasi ya zaidi ya kilomita 54 kwa saa zinavuma ndani ya kipenyo cha kilomita 650 kuelekea mashariki na ndani ya kipenyo cha kilomita 330 kuelekea magharibi ya kitovu cha kimbunga hicho.

Maofisa wa hali ya hewa wanasema kimbunga hicho kinaendelea kuwa kikali wakati kikielekea kaskazini magharibi.

Walisema kikiambatana na radi, mvua ya zaidi ya milimita 50 inaweza kunyesha kwa saa kwenye kitovu na maeneo ya upande wa kaskazini ya kimbunga hicho.

Maofisa wanatabiri kuwa mvua kubwa katika kipindi cha saa 24 itakuwa milimita 100 kwenye Pwani ya Pasifiki ya eneo la Tohoku, milimita 80 katika eneo la Kanto-Koshin na milimita 50 upande wa Tohoku kwenye Bahari ya Japani.

Kwa saa 24 hadi kesho asubuhi, milimita 100 hadi 150 za mvua huenda zikanyesha katika Pwani ya Pasifiki ya eneo la Tohoku, Kanto-Koshin, Hokuriku na mkoa wa Niigata.

Katika upande wa Tohoku kwenye Bahari ya Japani, milimita 50 hadi 100 za mvua zinatarajiwa kunyesha.