WASHINGTON, MAREKANI

KITUO cha kuzuwia na kudhibiti magonjwa nchini Marekani, CDC, kimesema kirusi kipya cha Corona aina ya Delta kinaweza kuambukiza kama vile ugonjwa wa tete kuwanga.

Gazeti la Washington Post ambalo limenukuu nyaraka za CDC lilisema kirusi hicho kipya cha Delta kinaweza kusababisha ugonjwa mkali zaidi.

CDC

Ripoti ya CDC iliyochapishwa kwenye tovuti ya Washington Post, ilisema kirusi kilichojibadili cha Delta, kinaweza kuvunja ulinzi unaotolewa na chanjo, lakini mamlaka hiyo ya afya ikaongeza kuwa haya ni matukio ya nadra.

Ripoti hiyo ya CDC huenda ikachochea mjadala juu ya ulazima wa kuvaa barakoa pamoja na kuzingatia masharti mengine ya kiafya, hasa katika wakati ambapo nchi nyingi zinaendelea na kampeni ya chanjo na kulegeza baadhi ya vizuizi vya kudhibiti kusambaa kwa virusi vya Corona.