NA ABOUD MAHMOUD

WANAMAZOEZI wa klabu ya Kitambi Noma wanatarajiwa kuondoka visiwani humu kuelekea Mkoani Morogoro, kwa ajili ya kushiriki bonanza lililoandaliwa na Uluguru Jogging &Sports Club linalotarajiwa kufanyika Julai 31.

Akizungumza na Zanzibar Leo, Katibu Mtendaji wa klabu hiyo ambae pia ni kiongozi wa msafara, Mohammed Saleh Ameir alisema jumla ya wanamichezo 50 watashiriki bonanza hilo ambapo wanatarajia kuondoka visiwani humu mapema Julai 30.

Alisema wakiwa Mkoani Morogoro wanatarajia kukaa kwa muda wa siku tatu kwa ajili ya shughuli mbali mbali, za kimichezo na kijamii ambazo zimeandaliwa na wenyeji wao.

Mohammed alisema bonanza hilo linatarajiwa kushirikisha klabu zote tano ambazo zimo katika shirikisho la MUWAFAKI ambao ni Uluguru Jogging, Kitambi Noma, Faita Jogging, Wakali Jogging zote za Dar es Salaam na Muungano Jogging ya Dodoma.

“Wana Kitambi Noma tunatarajia kuungana na wenzetu tulioanzisha umoja wetu wa MUWAFAKI, katika bonanza linalotarajiwa kufanyika mkoani Morogoro,”alisema.