NA MWAJUMA JUMA

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya KMKM Ame Msimu amekiri kuwa mashindano ya Kagame, ambayo timu hiyo itashiriki yatakuwa magumu kwake kutokana na ubora wa timu zinazoshiriki.

Msimu aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi, ambae alitaka kujua maandalizi yao kuelekea mashindano hayo yatakayoanza Agosti 1-15 jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo alisema licha ya ugumu wake watapambana ili kufikia hatua ya robo fainali na baadae, kuitafuta nusu fainali na fainali ili kutwaa ubingwa.

“Timu zote ambazo zimethibitisha ni mabingwa katika nchi zao,hivyo lazima tujipange ili kwenda kupambana”, alisema Msimu.

Sambamba na hayo aliwaomba wazanzibari kuiombea timu yao ili iweze kufanya vizuri kwenye mashindano hayo.

KMKM imepangwa kundi A pamoja na KCCA kutokea Uganda na Le Messager Ngozi ya Burundi.

Kundi B limejumuisha Azam FC kutoka Tanzania bara, Altabara ya Sudan na Tusker FC ya Kenya ambapo Kundi C, Yanga kutoka Tanzania bara imepangwa na Nyasa Big Bullets ya Malawi na Express FC kutoka Uganda.

Jumla ya timu 10 zitashiriki ambapo Tanzania Bara itatoa timu mbili Yanga na Azam, Altabara FC ya Sudan Kusini, Le Massager Ngozi ya Burundi, APR ya Rwanda, Express na KCCA za Uganda, Tusker ya Kenya na Big Bullets kutoka Malawi ambayo imealikwa.