NA ABOUD MAHMOUD

BAADA ya kilio cha muda mrefu kwa madereva wa vyombo vya moto maarufu kwa jina la Bajaji na Bodaboda kutaka watambulike na kufanya kazi zao wakiwa huru kimesikika.

Hivi karibuni kupitia vyombo vya habari, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Rahma Kassim Ali alitangaza rasmi kurasimisha usafiri huo kuwa ni moja ya biashara inayotambulika.

Kwa mujibu wa uwezo aliopewa waziri huyo chini ya kifungu cha 48(4) cha usafiri wa barabarani namba 7 ya mwaka 2003 aliweza kurasimisha usafiri huo wa bodaboda kwa kundi (B) na bajaji kuwa kundi (J).

Katika kauli iliyotolewa na Waziri huyo ilieleza kwamba hizi ni miongoni mwa ajira 300,000 alizozitaja Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Mwinyi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Ni jambo la faraja na linahitaji kupongezwa kutokana na vijana wengi ambao wamefanikiwa kujiajiri kupitia vyombo hivyo vya moto na kupata kipato ambacho kinawasaidia kuendesha maisha yao.

Kwa hakika usafiri wa bodaboda na bajaji umekua maarufu kati nchi mbali mbali hususan katika nchi zetu za Afrika ambazo kwa njia moja ama nyengine humsaidia dereva ambao wengi wao ni vijana kujikimu katika kutafuta riziki ya halali.

Hata hapa nyumbani Zanzibar vijana wengi wamejikita katika biashara hiyo na wanaendesha maisha yao kupitia biashara hiyo ambayo hivi sasa imekua ni kimbilio la wateja wengi wasiokuwa na uwezo wa kukodi taksi.

Lengo langu sio kusifia bali ni kutoa angalizo kwa waendesha biashara hizo kuwa makini na vitendo mbali mbali viovu vinavyosemekana kufanywa na baadhi yao.

Kuna mambo mengi yamekua yakilalamikiwa na wananchi na kutokea kwa matukio mbali mbali na yanayosikitishwa ambayo hufanywa na baadhi ya waendeshaji bodaboda wasiowaaminifu na kuleta madhara kwa jamii husika.

Miongoni mwa matukio tulioyashuhudia kufanyika kupitia usafiri huo ni pamoja na mwendo wa kasi ambao husababisha ajali nyingi na hata kutokea kwa vifo kwa madereva na abiria.