NA ABOUD MAHMOUD
WANANCHI wa Wilaya ya Kati Unguja wamesema ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi aliyoifanya hivi karibuni wilayani humo imeongeza matumaini ya kutekelezwa kwa ahadi alizozitoa kwa wananchi hao.
Waliyasema hayo hivi karibuni katika maeneo mbali mbali ya wilaya hiyo walipozungumza na mwandishi wa habari hizi na kueleza kuwa ingawa viongozi wengine wa ngazi tofauti walikua wanakwenda na kuwapa moyo wa kutatuliwa changamoto zinazowakabili, lakini kufika kwake kumewapa matumaini zaidi.
“Nimefurahishwa sana na ujio wa Dk. Mwinyi (Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi) ni faraja kwetu na imani yangu kuja kwake kutaweza kutatua kwa haraka changamoto zinazotukabili kwa muda mrefu,” alisema Omar Khatib mkaazi wa Mgeni Haji.
Naye Waziri Kitwana (69) mkaazi kutoka shehia ya Ubago alisema ameridhishwa na maelezo ya Dk. Mwinyi juu ya mzozo wa ardhi kati yao na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), lilikuwa linamkosesha raha lakini mara baada ya kufika Dk. Mwinyi na kuzungumza nao amejengewa imani ya kuondokana na tatizo hilo.
Alisema kutokana na kauli ya Dk. Mwinyi kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo wananchi wa kijiji hicho wamekua na matumaini na kuondokana na wasiwasi waliokuwa nao.
“Mimi na wenzangu tunaoishi hapa Ubago tulikua hatuna amani hata tukiambiwa na mtu yoyote tunaona tunadanganywa lakini kauli aliyoitoa Rais wetu ya kusema atalishughulikia na kulitafutia ufumbuzi imetupa moyo wa matumaini na wasiwasi umetuondoka,” alisema Kitwana.
Naye Fatma Kessi mkaazi wa Unguja Ukuu alisema kwa muda mrefu katika eneo lao kumekuwa na tatizo la maji hali ambayo ilikua inawapa wakati mgumu.
Alisema tatizo hilo ambalo limedumu kwa kipindi kikubwa na kukosa matumaini ya kupatiwa ufumbuzi wa suala hilo hivyo alisema ziara ya Dk. Mwinyi imewapa moyo wa kuondosha kilio chao.