NA ABOUD MAHMOUD
NENO burudani moja kwa moja hufahamika ni kitu ambacho humfurahisha mtu, kikundi au jamii kwa ujumla katika kuifurahisha nafsi .
Burudani zipo za aina nyingi ikiwemo michezo, ngoma za asili, muziki wa kisasa na mengine mengi, ambapo kila binadamu huelekeza mapenzi yake katika upande anaoupenda.
Kwa upande wa burudani ya ngoma ambazo zipo za aina mbali mbali, nazo zimeonekana kushamiri kwa kuwa na kundi kubwa na wapenzi wa fani hiyo.
Utamaduni wa kupenda burudani hizo hutokana na mambo mbali mbali, ikiwemo ustadi wa upigaji wa ngoma, lugha inayotumika na hata uchezaji wake.
Kupitia hayo yote yameonesha kuwa burudani ni moja ya kioo ambacho huangaliwa na wengi na kuitangaza nchi kitaifa na kimataifa .
Lengo la kuandika uchambuzi huu sio kuelezea maana ya burudani, bali kuelimishana umuhimu wake na nini kifanyike, katika kufika malengo tulioyakusudia katika kukuza na kutangaza utamaduni wetu.
Hivi karibuni Baraza la Sanaa Sensa Filamu na Utamaduni (BASSFU), imeifungia ngoma ya utamaduni inayojulikana kwa jina la ‘Baikoko’.
Sababu ambazo zilitajwa kuifungia ngoma hiyo ni kwenda kinyume na maadili na utamaduni wa asili ya Kizanzibari.
Wengi wetu tunafahamu kuwa ngoma hiyo asili yake ni Mkoa wa Tanga na imekuwa maarufu kuchezwa katika shughuli mbali mbali ikiwemo harusi.
Ni dhahiri kuwa baikoko ni ngoma ambayo haiendani na maadili yetu kutokana na maudhui ya nyimbo zake uchezaji wake ambavyo vyote vinaonesha kuwa ni vya utovu wa nidhamu.
Kitendo kilichofanywa na BASSFU ni cha kupongezwa kwani kimeonesha dhahiri kuwa kazi za taasisi hiyo za kulinda na kuenzi utamaduni wetu zinafanyika.
Kutokana na hilo na hii ni nchi yetu sote ipo haja kwa wananchi kutoa taarifa katika chombo hicho, kilichowekwa na Serikali endapo watathibitisha kuwepo kwa ngoma au burudani yoyote ambayo haiendani na maadili ya Kitanzania au Kizanzibari.
Imani yangu kwamba kama jamii itashirikiana kikamilifu na BASSFU katika kuondosha upotoshaji wa mila na desturi zetu kizazi kijacho kitafaidi na kurithi vyema utamaduni wetu.
Hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha kwa pamoja tunalinda mila, silka na utamaduni wetu, pamoja na kuondosha vitendo vinavyoashirikia kuharibu burudani zetu kama zilizofanywa na ngoma ya baikoko.
Tufahamu kwamba BASSFU ni chombo kilichoekwa na Serikali lakini kinahitaji mashirikiano makubwa kutoka kwa wananchi ili kiweze kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi.