KWA muda wa takriban miaka mitatu taarifa kutoka nchini Kenya zinaeleza kuwa kuna maelewano finyu baina ya rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta na naibu wake, William Ruto.
Uthibitisho kwamba viongozi hao wakuu nchini Kenya picha haziende sawa unaonesha kwenye matukio mbalimbali na hata kupisha mbali sana kupitia kauli zao.
Tofauti baina ya Kenyatta na Ruto zilianza kuonekana mnamo mwezi Machi mwaka 2018, pale rais Kenyatta alipozika uhasama baina yake na kiongozi wa upinzani wa muda mrefu nchini humo, Raila Odinga.
Mara tu baada ya rais Kenyatta na Odinga kuzika uhasama wao uliotokana na siasa za nchi hiyo, Kenyatta aliibuka na kuanza kumshutumu naibu wake kwa kuanza kampeni mapema mno za kutaka kurithi nafasi yake.
Hoja za Kenyatta kwenye shutuma dhidi ya Ruto, zilitokana na naibu rais huyo kuweka ahadi za kutekeleza miradi mikubwa kwa wananchi wa Kenya.
Kwa upande mwingine, naibu Ruto aliiona hatua ya Kenyatta kufikia makubaliano na Odinga ambao ni kinyume na makubaliano ya mwaka 2013, ni kama njama ya kumuondoa kwenye mbio za kuwania urais wa nchi hiyo.
Katika chama cha Jubilee ambacho kiliundwa mwezi Septemba mwaka 2016, uhusiano kati ya Kenyatta na naibu ambao ni viongozi wakuu wa chama hicho umedorora sana kiasi cha kudhofishwa nguvu za kisiasa za chama hicho.
Kenyatta na Ruto ndio walioafikiana kuunda chama cha Jubilee kwa pamoja ili kuwa na muungano wa chama cha siasa wenye nguvu kisiasa, hata hivyo hali ilivyo hivi sasa inaonekana kama vile Roto ambaye ni mshirika muasisi wa Jubilee anatengwa.
Wachambuzi wanaeleza kuwa mvutano wa ndani uliopo ndani ya chama cha Jubilee unatokana na suala la vita dhidi ya ufisadi, ambapo kinachohudiwa baadhi ya wafuasi wa Kenyatta wakigawanyika kwa wengine kumuunga mkono Ruto.
Wakati chama cha Jubilee kupitia kwenye hali hiyo, wafusi wa chama cha upinzani cha Orange Democratic Movement (ODM), kwa nguvu moja wanamtetea Kenyatta kutokana na shutuma za wanajubilee.
Kwa maana hiyo Raila Odinga ambaye ni kiongozi wa ODM, amekuwa mtetezi wa Kenyatta huku Ruto akionekana kuongoza upinzani ndani ya chama tawala cha Jubilee.
Kenyatta ameunda muungano mpya akitumia wapinzani wa kisiasa wa Ruto akimleta karibu kiongozi wa upinzani Odinga wa chama cha Orange Democratic Movement(ODM), kinara wa Wiper Democratic Movement (WDM) Kalonzo Musyoka, Gideon Moi wa Kanu na Isaac Ruto wa chama cha Mashinani.
Ushirikiano huu na vyama vingine umesababisha fujo katika vyama vya upinzani nchini Kenya, huku vyama vingine vikijaribu kusimama imara hasa katika ngome zao za kisiasa.
Kwa mfano chama cha Ford-K kimekumbwa na migogoro ya kiusimamizi ya ndani kwa ndani na mpaka sasa kina viongozi wawili. Makundi mawili ya uongozi yako mahakamani kupigania uongozi wa chama cha Fork-K.
Hali hiyo ndiyo iliyosababisha Kenyatta kuchukua usimamizi thabiti wa bunge la kitaifa na lile la seneti ambapo kwa sasa mabunge haya hayana upande wa upinzani.
Naibu wa spika wa bunge la seneti, kiongozi wa wengi na kamati zake zimefanyiwa mabadiliko makubwa. Hali hiyo imekumba bunge la kitaifa ambapo kiongozi wa wengi na naibu wake na kamati zake pia zimefanyiwa mchujo, ambapo hali hiyo mpya inatishia uhuru wa bunge katika utendaji kazi wake.
Miungano mipya katika siasa za Kenya ina misingi yake katika uhusiano kati ya Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga na huenda pia ikakumbwa na mitetemeko zaidi huku viongozi hawa wawili wakiweka mipango wa kura ya maamuzi kuhusu katiba ya Kenya.
Mipango na kampeni kuhusiana na mabadiliko ya katiba ilisambaratika kutokana na mripuko wa ugonjwa wa corona, ambapo rais Kenyatta na Raila Odinga wakisisitiza kuwa bado mipango hiyo ipo.
Kwa William Ruto, kuondolewa kwa wandani wake katika nyadhifa mbali mbali kunamaanisha kuwa ni bayana kwamba makubaliano yake na Kenyatta ya mwaka wa 2013 ambayo yangemfanya kumrithi Kenyatta kama rais wa tano wa Kenya, hayapo tena.
Hali hiyo inamfanya Ruto abadilishe mkakati mingine kama bado ana nia ya kuwania urais, hata hivyo anaweza kupata nguvu kutokana na kutoelewana kwa kundi kubwa lililoletwa pamoja na rais Kenyatta.
Mgogoro na uhusiano baina ya Kenyatta na naibu wake huenda ukakubwa na matatizo zaidi iwapo mpango wa marekebisho ya katiba utaanza hivi karibuni.
Ruto anasema kwamba hakuna dharura katika kuifanyia marekebisho katiba ya Kenya na kwamba fikra ya kutaka kuipanua serikali hasa katika ngazi na nyadhifa za juu kupitia kwa marekebisho haya ni jambo lisilofaa.
Wengi wanaamini kwamba Ruto amekasirishwa na kuvunjwa moyo baada ya kugundua kwamba Kenyatta huenda asimuunge mkono katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.
Hali hiyo imesababisha kuibuka kwa maswali kama chama cha Jubilee kitakuwa imara hadi uchaguzi wa mwaka wa 2022, ambapo kukiwa na taarifa kwamba huenda Ruto akakihama chama hicho ambacho amedai hakina udhabiti na kimetekwa nyara na matapeli wa kisiasa.
Ruto amedokeza kuwa huenda akaongoza upande utakaopinga kura ya marekebisho ya katiba ya Kenya huku akikejeli wanaounga mkono suala la mabadiliko ya katiba hiyo.
“Hata sijui ni nini kitakachobadilishwa…kulingana na ufahamu wangu, mabadiliko haya yanasukumwa na viongozi, si wananchi. Wananchi kwa sasa wanashughulishwa na ukosefu wa ajira na mambo mengine ya kimsingi katika maisha yao”, alisema Ruto.
Kwa upande wake, Kenyatta alisisitiza kwamba kura ya mabadiliko ya katiba ni lazima kufanyika ili kuondoa hali ya wasiwasi ambayo huikumba Kenya kabla na baada ya uchaguzi mkuu kwa sababu ya jamii fulani kuhisi kutengwa kutoka kwa uongozi wa taifa.
Rais Kenyata amekuwa akieleza kuwa ana maono ya kulipokeza taifa hali ya mshikamano na umoja kupitia mchakato wa BBI, ambao utakuwa sehemu ya jinsi atakavyokumbukwa akiondoka mamlakani.
Lakini naibu wake anahoji kuwa mabadiliko ya kikatiba hayawezi kufanywa kuwa jinsi kiongozi yeyote atakavyokumbukwa. “Mabadiliko ya kikatiba si jambo tunaloweza kuamua kama chama- ni kwa Wakenya wote kuamua”, alisema Ruto.
Itakumbukwa kwamba mnamo mwaka wa 2005, rais mstaafu Mwai Kibaki aliwatimua Raila Odinga na wandani wake kwa kuongoza upinzani dhidi ya katiba iliyopendekezwa wakati huo.
Hata hivyo, kulingana na katiba ya Kenya ya sasa, rais Kenyatta hana uwezo wa kumtimua naibu wake kutoka wadhifa wake, lakini anaweza kuchukua hatua na kufanya mabadiliko katika serikali kwa jumla na kumpunguzia uwezo wake.
Ili rais wa Kenya aweze kumuondoa kwenye nafasi yake naibu wake basi anaweza kuanzisha mswaada wa kutokuwa na imani na naibu wake na kuuwasilisha bungeni kwa ajili ya maamuzi.
Kwa muda mrefu, Ruto amekwepa kumshutumu Kenyatta hadharani, lakini katika siku za hivi karibuni yeye na wandani wake wanaonekana kumshutumu Kenyatta moja kwa moja hadharani.
Kwa mfano, wabunge wawili ambao ni wandani wa Ruto wametoa matamshi ya kumshutumu Kenyatta na mama yake, Ngina Kenyatta, kwa wamechangia sana matatizo yanayowakumbwa wananchi wa Kenya.
Wengi wanaamini kwamba msukosuko uliopo katika chama cha Jubilee na uhusiano unaoendelea kudorora baina ya Kenyatta na naibu wake ni mipango ya Ruto ya kuondoka kwenye serikali na kulenga kampeni zake za uchaguzi wa mwaka 2022.
Katika siku za hivi karibuni, Ruto amekuwa akifanya mikutano nyumbani kwake na mingine katika maeneo mbali mbali nchini Kenya ambapo amechagia harambee za mamilioni kwa vijana na makundi ya akina mama.
Pia, amekuwa na mikutano na viongozi mbali mbali wa makanisa na washawishi wengine akionekana kupanga kampeini bila kumtegemea Rais Kenyatta.
Aidha, baadhi ya viongozi wanaomuunga mkono Ruto wamekuwa wakimrushia cheche za maneno Kenyatta wakimshutumu kwa kumtenga kutoka shughuli muhimu za chama cha Jubilee, serikali na kutomuunga mkono naibu wake kisiasa.
Ruto ameshutumiwa na baadhi ya wanasiasa ambao wanatilia shaka ukosoaji wake wa serikali ambayo bado yeye ndiye naibu wa Rais.
Kilicho wazi katika siasa za Kenya ni kuwa uhusiano baina ya Rais Kenyatta na naibu wake katika chama tawala cha Jubilee na serikali kwa jumla unakumbwa na wakati mgumu hasa nchi inapojishughulisha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.