CAPE TOWN, AFRIKA KUSINI

WAZIRI wa sheria wa Afrika Kusini Ronald Lamola amesema rais wa zamani wa nchi hiyo Jacob Zuma ambaye ameanza kutumikia kifungo chake cha miezi 15 jela anaweza kustahiki msamaha na kuondoka jela baada ya miezi minne.

Waziri Lamola amewaambia waandishi wa habari kuwa Zuma atawekwa karantini kwa siku 14 kwa kuzingatia kanuni za kupambana na ugonjwa wa Covid-19.

Ameongeza kuwa chini ya kanuni za idara ya magereza za Afrika Kusini, Zuma atastahiki kupata msamaha mara baada ya kutumikia robo ya muda wa kifungo chake.

Aidha Lamola amesema Zuma atalindiwa heshima yake katika kipindi chote atakachokaa gerezani.

Rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini mwenye umri wa miaka 79 alijisalimisha mwenyewe kwa polisi na kupelekwa gereza la mkoa wa KwaZulu-Natal.

Chama tawala cha Afrika Kusini cha African National Congress, ambacho kiliwahi kuongozwa na Zuma, kimesema katika taarifa kuwa kinaheshimu uamuzi wake wa kutii sheria na kwamba ni jambo la ujasiri na uamuzi mgumu.