Simba ikitetea kombe la ASFC

NA MWANDISHI WETU

SIMBA imetwaa  ubingwa  wa Kombe la Shirikisho kwa mara ya tatu mfulululizo baada ya kuwafunga watani wao wa jadi Yanga bao 1-0.

Mchezo wa fainali ulipigwa katika uwanja wa Lake Tanganyika  Kigoma ambao ulihudhuriwa na mashabiki wengi, unahitimisha msimu wa ligi ya Tanzania Bara mwaka huu.

Mchezo huo uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa timu zote, ulianza kwa kila timu kucheza kwa tahadhari kubwa kila mmoja akichelea kufungwa bao la mapema.

Mchezo huo uliendelea kuwa wa kushambuliana kwa zamu kila mmoja akijaribu kusaka bao kwa mwenzake, lakini washambuliaji wa timu zote walikosa mabao na hadi dakika 45 za kipindi cha zinamalizika hakuna timu iliyoweza kuona lango la mwenzake.

Hata hivyo katika kipindi cha kwanza Yanga walipata pigo kubwa baada ya kiungo wake  Mukoko Tonombe raia wa Congo kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumpiga kiwiko nahodha wa Simba John Bocco dakika ya 43.

Kipindi cha pili Simba ilitawala zaidi mchezo huko Yanga wakicheza kwa kujilinda, jambo ambalo liliwafanya Simba kupeleka mashambulizi mengi langoni mwa Yanga.

Kiungo wa Simba Taddeo Lwanga  ndiye aliyepeleka machungu huko Jangwani baada ya kupachika bao hilo pekee la ushindi dakika ya 80.

Lwanga alifunga bao hilo kwa kichwa akimalizia mpira wa kona uliopigwa na kiungo wa kimafaifa wa Msumbiji, Jose Luis ambaye jana ilikuwa siku yake ya kuzaliwa.

Kuingia kwa bao hilo Yanga walizinduka na kuanza kufunguka wakisaka bao la kusawazisha lakini ukuta wa Simba, ulikaa imara na kuzuwia mashabumbulizi yote yalioelekezwa langoni mwao na mpaka dakika 90 zinamalizika Simba ikifanikiwa kutoka na ushindi huo.

Ni taji la pili mfululizo la ASFC kwa Simba SC na taji la tatu la msimu, baada ya kubeba Ngao ya Jamii na ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara mapema mwezi huu.