NA ABDI SULEIMAN

IKIWA serikali ya SMT na SMZ, zimeanza kuchukua juhudi za kukabiliana na wimbo la tatu la maradhi ya Covid 19, viongozi wa serikali Kisiwani Pemba, wamesema kuwa tayari mikakati mbali mbali imeshaanza kuchukulia katika kukabiliana na maradhi hayo.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tafauti kwa njia ya simu, wamesema kuwa moja ya mikakati hiyo ni kusambaza kwa vifaa vya kunawiya mikono katika maeneo yenye mikusanyiko.

Mkuu wa mkoa wa Maskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatib, alisema miongoni mwa mikakati ambayo wameanza kuichukua ni kuwapatia elimu wananchi juu ya kujikinga na wimbi la tatu la Covid 19, inayoendelea duniani na barani Afrika.

“Tumeanza na vitakasa mikono, ndoo zenye maji ya kutiririka, kuweka katika maeneo yenye watu wengi, ikiwemo sokoni, stendi za gari hata katika hospitali zetu, lengo ni kudhibiti maambukizi ya janga la Covid 19”alisema.

Aidha aliwataka wananchi kutokudharau au kupuuza maelekezo yote wanayopatiwa na serikali, pamoja na wataalamu wa afya katika kujikinga na ugonjwa huo.

Mkuu huyo wa Mkoa aliwashauri wananchi wanapohitaji huduma za afya, kutumia vituo vilivyokaribu navyo kwa lengo la kuepusha msongamano wa watu kwenye hospitali za Wilaya.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Masoud, alisema wanatarajia kukutana hivi karibuni na watendaji wa wizara ya afya, kwa ajili kuona hatua na mikakati watakayoichukua katika kukabiliana na wimbi la janga la Covidi 19.

“Maagizo na mikakati yoyote yatakayotolewa na wataalamu wetu wa afya, inapaswa kutekelezwa tena kwa nguvu zote ili kuona tunadhibiti hali hiyo”alisema.