NA MARYAM HASSAN
MAAHIRISHO yasiyo na sababu yanayotolewa na upande wa mashitaka, katika kesi ya kupatikana na dawa za kulevya kila inapofikishwa mahakamani kwa ajili ya kusikilizwa, yamemchosha mshitakiwa wa kesi hiyo na kuiomba mahakama kumwondelea kesi hiyo.
Mshitakiwa wa kesi hiyo ni Hamza Abdalla Rikungwa (25) mkaazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam, aliwasilisha ombi hilo mbele ya Hakimu Said Hemed Khalfan wa mahakama ya mkoa Mwera, wakati kesi hiyo lilipofikishwa kwa ajili ya kusikilizwa.
Likiwa mahakamani hapo, upande wa mashitaka unaosimamia kesi hiyo, ulidai haujapokea shahidi na kuomba iahirishwe na kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa.
Ombi hilo la upande wa mashitaka, lilipingwa na mshitakiwa huyo na kuiomba mahakama kuiondoa kesi hiyo, kutokana na kauli hizo ni za muda mrefu na hazina msingi.
Akiwasilisha ombi hilo, mshitakiwa huyo alidai kwamba, ni muda mrefu shauri hilo lifikishwa mahakamani hapo limekuwa likiahirishwa na upande wa mashitaka, kwa kisingizio cha ukosefu wa mashahidi.
Hivyo alisema, ni vyema shauri hilo likaondolewa kwa kuwa upande wa mashitaka hauna nia ya kuleta mashahidi.
Mara baada ya kutoa ombi hilo, Hakimu Said, alikubaliana nae na kuliondoa shauri hilo, huku akieleza kuwa maahirisho katika shauri hilo yamekuwa hayana mwisho.
Hamza, alifikishwa mahakamani hapo kosa la kupatikana na dawa za kulevya, kosa ambalo alidaiwa kulitenda Januari 19 mwaka 2019 majira ya saa 6:30 za usiku, huko Paje wilaya ya Kusini mkoa wa Kusini Unguja.
Mshitakiwa huyo, alidaiwa kupatikana na begi lenye rangi nyeusi ndani yake mkiwa na mifuko miwili ya nailoni yenye rangi nyeusi, ikiwa na bangi nyongo 2,591 zenye uzito wa gramu 1.625 jambo ambalo ni kosa kisheria.
Hadi kesi hiyo inaondolewa mahakamani hapo, ilikuwa tayari imeshasikilizwa shahidi mmoja tu, huku mashahidi wengine ‘wakiingia mitini’ baada ya kupokea wito wa mahakama.