Zaspoti

MSIMU wa Ligi Kuu ya Zanzibar 2020/2021 umekamilika KMKM kutangazwa mabingwa wa michuano hiyo mikubwa visiwani hapa.
Baada ya kumalizika kwa ligi hiyo, kinachufuata sasa ni zoezi la uhamisho na usajili kwa ajili ya msimu mpya.
Tayari klabu kadhaa zimekuwa kwenye mchakato wa usajili ingawa haujawa rasmi, lakini, hilo ni katika kuhakikisha zinakuwa na vikosi imara kwa ajili ya ngarambe hizo zenye kila ya aina ya ushindani.

Ni msimu ambao tunatarajia kuwa na ushindani kama ilivyokuwa msimu ambao ulimalizika kwa KMKM kutangazwa mabingwa wapya.
Hivyo tunaamini kuwa msimu ujao nao utakuwa wenye msisimko mkubwa na klabu zinatakiwa kutumia muda huu mfupi uliobakia kujiandaa kwa ajili ya msimu huo na sio kusuburi dakika za mwisho ndio kuanza maandalizi.
Wataalamu wa michezo wakati wote wamekuwa na falsafa ya kuamini kwamba klabu inayokuwa na maandalizi mazuri ya msimu pia inayojingea mazingira bora ya ubingwa mwishoni mwa msimu.

Kwa mantiki hiyo, timu zinatakiwa kuanza kujipanga mapema ili ligi inapoaanza ziwe kwenye moto na kujiwekea mazingira mazuri badala ya kusubiri dakika za mwisho ndio zianze kupambana ili kukwepa kushuka daraja.
Hilo tumelishuhudia msimu uliopita ambapo timu za Pemba zilijikuta zikitapia roho bila ya mafanikio kushuka daraja na hatimaye zikashindwa na hivyo kuondoka kwenye ligi hiyo yenye hadhi ya kipekee kama ngazi ya juu.

Hivyo, ni matarajio ya mashabiki wengi wa soka kuona msimu ujao unakuwa bora kuanzia kwa timu kuwa bora na waamuzi kuchezesha kwa kufuata kikamilifu sheria 17 zinazotawala mchezo wa soka.
Msimu uliopita baadhi ya waamuzi walitajwa kutokuwa makini kwenye usimamizi huo na hivyo kupelekea lawama kwa baadhi ya klabu.

Ili kuepuka hilo, Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), kwa kushirikiana na Kamati ya Waamuzi Zanzibar kufanya jitihada za kuwapiga msasa waamuzi ili msimu ujao uwe wenye mafanikio zaidi.
Ligi ikiwa na ushindani wa kweli sio ule wa baadhi ya timu kubebwa au kutokuwa washindani, kunapelekea kushusha kwa ubora wa ligi na pia kiwango cha taifa kwa ujumla.

Lakini pia kunapokuwepo na ushindani wa ligi pia utasaidia kuvutia wadhamini ambao hutoa fedha kwa ajili ya kuiongezea ushindani sawa na wao wenyewe kujitangaza kibiashara kupitia mchezo huo wa soka.

Kutokana na hilo, tunaamini hivi sasa ni wakati muafaka kwa klabu kuanza kujiandaa kwa msimu mpya ili kuongeza chachu ya ushindani katika ligi hiyo.
Kwa kipindi kirefu sasa Ligi Kuu ya Zanzibar imekuwa ikichezwa bila ya udhamini, labda kutokana na mfumo uliokuwepo kabla ambao pia ulichangiwa na idadi kubwa ya timu shiriki.

Lakini tunaamini kwa mfumo wa sasa, udhamini unawezekana baada ya mabadiliko ya kimfumo kwa kuwa na idadi ndogo ya klabu kwenye ligi hiyo.
Sasa tufikie mahali na kuliona hili ni letu sote kwa njia moja au nyengine ili siku ya mwisho ligi yetu iwe na udhamini utakaongeza chachu ya mafanikio kwa ajili ya vijana wetu wa baadaye.
Zanzibar yenye mafanikio ya soka inawezekana.