WAWAKILI wa Zanzibar kwenye michuano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), tayari wameshapatakina baada ya kukamilika kwa Ligi Kuu ya Zanzibar na Kombe la FA msimu huu.

Baada ya KMKM kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Zanzibar na kukata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, maafande wenzao wa Mafunzo wao wamejihakishia kushiriki Kombe la Shirikisho.

Tunachukua nafasi hii kuzitakia kila la heri timu hizo ziweze kufanya vyema kwenye michuano hiyo ya kimataifa, zikiwa na taswira ya kushindana badala ya kushiriki pekee.

Sote tunaelewa kuwa patashika za michuano hiyo ni ngumu na zenye kuhitaji maandalizi ya mapema katika kukabiliana nazo na hilo tunaamini litafanyika kwa wawakilishi wetu hao.

Kutokana na hali hiyo, ni imani yetu kwamba KMKM na Mafunzo mnatakiwa kuanza maandalizi sasa badala ya kusubiri ratiba itolewe, kwani kufanya hivyo ni sawa na kutozitendea haki nafasi hizo.

Kwa kipindi kirefu, ushiriki wa Zanzibar kwenye michuano ya Afrika haujakuwa mzuri na kumekuwepo na dhana iliyojengeka miongoni mwa mashabiki kuwa timu zetu haziwezi kuvuka raundi za mwanzo za michuano hiyo ya kimataifa.

Hivyo, tunazishauri KMKM na Mafunzo zitambue kuwa zinakabiliwa na kibarua kigumu cha kurudisha imani za mashabiki na kuondoa dhana hiyo potofu ambayo kwa njia moja au inaharibu mustakala bora wa soka yetu.

Na hilo litaweza kuondoka kwa kufanya maandalizi ya mapema ya kimkakati sambamba na kujielewa kwa wachezaji kwenye jukumu la wajibu wa kujituma mchezoni.

Zanzibar Leo tunaamini wachezaji na mabenchi ya ufundi ya wawakilishi wetu hao wanalielewa hilo na kamwe hayatakuwa tayari kusubiri maandalizi ya kushtukuiza baada ya kuwekwa hazarani kwa ratiba.

Kama ambavyo tunatarajia kuona kutoka kwenu uwakilishi bora kwenye michuano hiyo, lakini, pia mkumbuke jukumu kubwa litakalokuwa mmelibeba kwenye kupeperusha bendera ya Zanzibar kimataifa.

Kubwa tunalowaambia ni kwamba mnakwenda kwenye michuano hiyo kwa niaba ya Wazanzibari wote na hivyo mnatakiwa kupambana.a

Mbali na kuiletea nchi sifa, michuano hiyo ni nafasi nyengine kwa wachezaji wa Zanzibar kutangaza vipaji vyao na hatimaye kuzivutia klabu mbalimbali za nje ili kuwasajili.

Kufanya vizuri kwa timu za Zanzibar kwenye mashindano hayo kutarejesha imani ya mashabiki wa soka nchini baada ya kipindi kirefu cha kuondolewa mapema sambamba na kukosa aina fulani ya ushindi kama yalivyo mataifa yanayoinukia kwenye mchezo huo.

Hivyo tunazitakia kila la heri KMKM na Mafunzo kuelekea michuano hiyo yenye hadhi kubwa ngazi ya klabu barani Afrika.

Zanzibar yenye mafanikio ya kimichezo inawezekana ikiwa kila mmoja wetu atatimiza wajibu wake.