Ni kwa kusaidia amani akiwa waziri wa ulinzi

NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ametunukiwa tuzo ya juu ya heshima inayofahamika kama “Legion d’ Honner” kutoka kwa rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron.

Dk. Mwinyi alitunukiwa tuzo hiyo jana na balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Frederic Clavier kwa niaba ya rais Emmanuel Macron, tukio lililofanyika katika ukumbi wa ikulu jijini Zanzibar.

Akiwa na ujumbe wake, balozi huyo alisema Dk. Mwinyi anastahiki kupatiwa tuzo hiyo kutokana na mchango wake wakati akiwa waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa la Tanzania.

Dk. Mwinyi alitoa shukurani za dhati kwa rais Macron kwa kumtunuku tuzo hiyo iliyotokana na kuthamini mchango alioutoa wakati akiwa waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa la Tanzania takriban kwa miaka 10.

Alisema kuwa amepokea tuzo hiyo ambayo ni heshima kubwa kwani hutolewa kwa  watu mbali mbali duniani hasa kwa mchango wake unaopaswa kupewa heshima hiyo.

Alieleza kwamba takriban miaka 10 akiwa waziri wa Ulinzi wa Tanzania ambapo katika kipindi hicho serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaidia kwa kiasi kikubwa katika operesheni  tano za kudumisha amani hasa zile za Bara la Afrika.

Hivyo, Dk. Mwinyi alitoa shukurani kwa heshima hiyo na kueleza kwamba, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Jamhuri ya Ufaransa.

Dk. Mwinyi alisema kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kushirikiana na wafanyabiashara wa Ufaransa na taasisi mbali mbali za Ufaransa ili kuweza kuleta maendeleo kwa wananchi.

Alisisitiza kwamba amani na utulivu uliopo Zanzibar ni matokeo ya mazungumzo kati ya  vyama vya siasa vya Zanzibar ambavyo viliamua kujenga serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kuleta amani itakayoharakisha maendeleo ya haraka.