PARIS, UFARANSA

RAIS wa Ufaransa Emmanuel Macron atashiriki kwenye mkutano utaakowashirikisha viongozi wa mataifa ya G5 Sahel unaotarajiwa kufanyika kesho kwa njia ya video.

Awali kulikuwepo na mashaka kuhusu ushiriki wake, hata hivyo imethibitishwa rasmi kwamba rais Macron atashiriki katika mkutano huu. Mataifa ya G5 Sahel, yanaundwa na Burkina Faso, Chad, Mali, Mauritania na Niger.

Mkutano huo utakuwa ni maalum kwa sababu atakuwa pamoja na rais wa Niger Mohamed Bazoum pembeni yake.

Huu utakuwa ni mkutano wa kwanza wa rais wa Niger kushiriki na viongozi wa G5 Sahel kama mkuu wa nchi.

Macron na Bazoum wakiwa jijini Paris, wataungana moja kwa moja na wenzao kwenye mkutano huo ambao utagusia kwa undani suala la usalama katika ukanda huo unaokabiliwa na vikundi vya wapiganaji.

Itakuwa fursa kwa rais huyo wa Ufaransa kutoa mpango wa taifa hilo kwa nchi hizo za bara Afrika katika siku zijazo katika kupambana na makundi mbalimbali ya waasi wanaotishia harakati za kigaidi.

Mkutano huu unakuja takriban mwezi mmoja baada ya kutangazwa kumalizika kwa operesheni Barkhane huku Ufaransa ikitangaza kupunguza vikosi vyake kufikia Januari 2023.