PYINMANA, MYANMAR

JESHI la Myanmar limewakamata na kuwazuia madaktari kadhaa kutokana na kuunga mkono maandamano ya kupinga utawala wa  kijeshi ulilochukua madaraka ya kuliongoza taifa hilo.

Inaelezwa kuwa wengi waliozuiliwa ni madaktari wa hospital binafsi ambao ndio wanasaidia kwenye juhudi za kutibu wagonjwa wa corona, wakati taifa hilo likikabiliana na wimbi jipya la maambukizi.

Tangu jeshi lilipofanya mapinduzi dhidi ya utawala wa kiongozi wa kiraiya Aung San Suu Kyi mwezi Februari, ghasia na maandamano yaliyofuata yameathiri vita dhidi ya corona, wakati wanaharakati wakisema kuwa madaktari waliokamatwa ni kutokana na kupinga mapinduzi hayo.

Wiki hii Myanmar imetangaza visa vipya 6,000 vya corona baada ya kuripoti vifo 286 hapo awali.

Wauguzi pamoja na wafanyakazi wa vyumba vya kuhifadhia maiti wanasema kuwa idadi hiyo huenda ikawa kubwa zaidi kwa kuwa maeneo ya kuchoma miili yameelemewa.