TOKYO, JAPANI

KAMATI ya Urithi wa Dunia ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO imeyaongeza kwenye orodha yake, maeneo manne yaliyo mikoani Kagoshima na Okinawa.

Maeneo hayo ni Kisiwa cha Amami-Oshima, Kisiwa cha Tokunoshima, eneo la kaskazini la Kisiwa cha Okinawa, na Kisiwa cha Iriomote.

Serikali ya Japani imekuwa ikishinikiza kusajiliwa kwa hekta zipatazo 43,000 za misitu na wanyama pori kwenye visiwa hivyo.

Inasemekana misitu ni makaazi ya wanyama mbalimbali wa kiasili ikiwemo sungura wa Amami, paka wa Iriomote, na spishi ya ndege wajulikanao kama Yambaru Kuina, au Okinawa Rail.

Kamati hiyo itajadili iwapo iongeze kundi la maeneo ya akiolojia yaliyopo kwenye mikoa ya Hokkaido, Aomori, Iwate na Akita kaskazini mwa Japani kwenye orodha ya Urithi wa Dunia ya maeneo ya kitamaduni.