NA MWAJUMA JUMA

TIMU ya soka ya Mafunzo  imefanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano ya kombe la Shirikisho (FA) kwa ushindi wa penalti 4-3 katika mchezo wa fainali uliochezwa jana

Mchezo huo ambao uliwakutanisha mabingwa hao  dhidi ya KVZ ulivuta hisia za watazamaji walio wengi ulichezwa katika dimba la Amaani majira ya saa 10:00 za jioni.

Miamba hiyo ilipigiana mikwaju hiyo ya penalti baada ya dakika 90 kufungana bao 1-1.

Katika mchezo huo timu hizo zilikwenda mapumziko wakiwa wamefungana bao 1-1 huku KVZ ambao ndio waliokuwa wenyeji wakitangulia kupata bao.

KVZ walipata bao la kuongoza kupitia mchezaji wake Nassor Saleh na Mafunzo ambao baada ya miaka mitano wamekosa kushiriki kimataifa wakasawazisha kupitia kwa Abdulhakim Naimu.

Kuingia kwa mabao hayo kuliufanya mtanange huo kuzidi kushambuliana na mashabiki waliokuwa wakitumbuizwa na ngoma za beni na kidumbaki kutoka vikosi vyote viwili wakiburudika nao.

Kipindi cha pili kilikuwa cha amsha amsha hasa kwa Mafunzo kutokana na kukosa nafasi nyingi za wazi ambazo walizijutia.

Mgeni rasmi katika mchezo huo alikuwa ni  Mbunge wa Jimbo la Shaurimoyo Ali Raza ambae alikabidhi zawadi kwa mshindi wa mchezo huo.

Bingwa huyo ataiwakilisha Zanzibar katika kombe la Shirikisho Afrika, alikabidhiwa kombe na medali za dhahabu wakati mshindi wa pili alivishwa medali za fedha.