BEIJING, CHINA

WATAALAM wa hali ya hewa wamesema kuwa takriban ya watu 25 wamefariki kutokana na mafuriko kwenye jimbo la Henan katikati mwa nchi ya China kufuatia siku kadhaa za mvua kali, huku wakiendelea kutabiri kwamba mvua hizo zitaendelea kunyesha kwa siku tatu zaidi.

Ripoti zinaeleza kuwa barabara za mji mkuu wa jimbo hilo wa Zhengzhou zimesombwa na maji wakati madereva wakilazimika kutembea kwa miguu huku maji yakiwafika kiunoni, pia mafuriko hayo yamesomba njia za reli ambazo zinategemewa kwa usafiri na watu wengi nchini humo.

Inaelezwa kuwa watu 12 wamefariki kwenye vituo vya treni vya chini ya ardhi wakati takriban 500 waliokolewa kulingana na ripoti ya chombo cha habari cha serikali.

Aidha mabwawa pamoja na hifadhi nyingine za maji zinasemekana kujaa kutokana na mafuriko hayo wakati kukiwa na wasi wasi wa kuporomoka kwa bwawa la Yihetan lililoko karibu na mji wa Louyang.

Zaidi ya watu 100,000 wamepelekwa kwenye maeneo salama, huku wanajeshi pamoja na polisi wakisaidia kupeleka misaada ya kibinadamu kwa watu walioathiriwa