NAIROBI, KENYA

MAJAJI wawili wa mahakama kuu nchini Kenya, Aggrey Muchelule na Said Juma Chitembwe, wamekamatwa na maafisa wa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai, kwa madai ya kula rushwa kutokana na kesi walizo sikiliza awali jijini Nairobi.

Wawili hao walihojiwa kwa zaidi ya masaa mawili na baadae wakaachiwa huru, lakini wakili wao, Danstan Omari anaeleza kuwa ni mwendelezo wa hatua za serikali kuminya uhuru wa idara ya mahakama.

Hata hivyo makarani na madereva wanaofanya kazi kwenye ofisi za majaji hao walifikishwa katika idara ya upelelezi kuandikisha taarifa zao.

Muchelule ni mmoja wa majaji waliokosa kuteuliwa kwenye mahakama ya rufaa na rais Uhuru Kenyatta kwa madai ya kuwa na dosari za maadili.

Aidha pia ni miongoni mwa majaji sita kati ya 40 ambao rais Kenyatta hakupandisha vyeo alipofanya uteuzi huo mwezi Juni mwaka huu.

Japo vyombo vya habari vya Kenya vinanukuu maafisa wa upelelezi kuwa kuna masuala mazito wanayochunguza dhidi ya majaji hao wawili, huku wakili wao Danstan Omari akidai kuwa kuna maswala yasioeleweka..

Rais Kenyatta amekuwa akikabiliwa na shutuma nyingi juu ya kuteua majaji 34 na kuwaacha wengine sita bila kuweka wazi sababu za kufanya hivyo, na hii imeonekana kama uminyaji wa uhuru wa idara ya mahakama.

Muungano wa mahakimu tayari umeeleza kuwa Kenyatta hana uwezo kisheria wa kuchagua baadhi ya majaji huku akiwaacha wengine.