NA KHAMISUU ABDALLAH
WIZARA ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar, inakusudia kujenga mji wa kisasa katika eneo la Kilimani ili kuweka haiba nzuri ya eneo hilo.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Joseph Kilangi aliainisha mpango huo mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi wakati wa majumuisho ya ziara yake aliyoifanya katika Mkoa wa Mjini Magharibi hivi karibuni.
Alisema mji huo unakusudia kuwa na majengo marefu 10 kwa ajili ya makaazi ya wananchi ambayo yanatochukuwa wananchi zaidi ya 405 ambapo majengo manne kati yao watafidiwa wananchi waliopo katika eneo hilo na majengo mengine manne yatakuwa vitega uchumi kwa ajili ya kuingiza mapato katika shirika lake la nyumba.
“Wapo watu ambao wamepewa hati na kujenga nyumba za makaazi katika maeneo ya wazi na kuharibu mandhari ya mji huo kama ilivyokusudiwa na Rais wa kwanza Mzee Abeid Amani Karume ikiwemo kuwakosesha watoto kukosa maeneo ya kucheza,” alisema.
Alisema jengine lengo jengine la kusudio la kujengwa mji huo ni sehemu ya biashara yakiwemo mabenki na maduka ya kisasa ytakayosaidia kuweka mji huo kuwa mzuri.
Alisema wizara pia inakusudia kuweka hoteli ya nyota tano ambayo itakuwa karibu na pwani kwa kuingia mkataba na mwekezaji kwa ajili ya kumkodisha eneo ili kuwa sehemu ya kitega uchumi chake na kuweza kurejesha gharama aliyoingia katika ujenzi huo na kupata mapato kutokana na shughuli zinazotolewa katika hoteli hiyo.
Alisema tayari wizara imeshaanza kupima eneo hilo lenye ukubwa wa mita mraba 200,700 ambapo kwa sasa kuna majengo 16 na baadae kuja na michoro na baadae kupelekwa serikalini kwa ajili ya kuridhia na baadae kutoa tenda kwa ajili ya kujenga mji wa kisasa katika eneo hilo.
Sambamba na hayo, alisema lengo jengine ni kuugawa mji wa Zanzibar kwa watalii kuingia Mji Mkongwe na akitoka aweze kukuta mji wa kisasa kabla kuingia ng’ambo.
Hata hivyo, alisema ujenzi wa mji huo pia utakwenda sambamba na ujenzi wa msikiti wa kisasa ili kuweza kuwahudumia wakaazi wa maeneo hayo na maeneo jirani.