VALLETTA, MALTA

MATOKEO ya uchunguzi huru wa mauaji ya mwandishi wa habari Daphne Caruana Galizia yaliyotolewa yamedhihirisha kuwa serikali ya Malta inapaswa kubeba dhamana la mauaji hayo kutokana na utamaduni wake wa kuwa na tabia ya kutokujali.

Familia ya Caruana Galizia ilianzisha uchunguzi huo kutaka kujua zaidi kuhusu mripuko wa bomu lilotegwa ndani ya gari uliotokea Oktoba 16, 2017 karibu na nyumba ya familia ya mwandishi habari huyo nchini Malta.

Uchunguzi huo uligundua kuwa hakuna ushahidi kwamba serikali inaweza kubebeshwa jukumu la moja kwa moja la mauaji hayo.

Serikali inapaswa kuwajibika kwa kutengeneza mazingira ya kutokujali, yanayotokana na usimamizi mbovu unaoanza kwenye ofisi ya waziri mkuu na kuenea hadi kwenye jeshi la polisi hali iliyodhoofisha nguvu ya utawala wa sheria.