WATAALAMU wanaendelea na tafiti kubaini mambo mbalimbai tusiyoyajua kuhusiana na miti, hata katika makala hii nakudokolea baadhi ya mambo ambayo yamebainika kwenye miti kutokana na tafiti mbalimbali.

Duniani inakadriwa kuna takriban miti trilioni tatu kulingana na utafiti uliofanywa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Yale. Utafiti huo umejumuisha spishi zipatazo 60,000 za miti.

Nusu ya spishi hizo zinazopatikana katika nchi moja pekee. Brazil, Colombia na Indonesia ni nchi ambazo kunapatikana idadi kubwa zaidi ya spishi za miti hiyo.

Miti hujing’oa na kuhama sehemu ilipo, lakini wingi wake unaweza kupungua kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Utafiti uliojumuisha spishi 86 za miti kutoka mwaka 1980 hadi 2015 mashariki mwa Marekani uimegundua kwamba asilimia 73 ya miti ilihamia magharibi mwa nchi ambako kunapatikana mvua kwa wingi. Kwa wastani, miti hiyo inasemekana kuwa ilihama kilomita 16 kila miaka 10.

Mbali na kwamba miti inatupa kivuli, inaweza pia kupunguza joto linapokuwa kali. Inafanya hivyo kwa kunyonya mionzi ya jua na kutoa maji hewani kupitia majani yake. Kawaida sehemu za mijini huwa na joto kali sana wakati wa kiangazi.

Lakini utafiti wa mwaka 2019 uliofanywa Marekani umeonyesha kwamba, miti inapofunika asilimia 40 ya mji, wakati wa kiangazi joto linaweza kupungua kwa nyuzi joto 5.

Miti inafyonza gesi ya kaboni iliyo hewani na hivyo ina umuhimu sana katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Majani pia huchuja gesi zenye sumu zinazochafua hewa kama vile dioksidi ya nitrojeni na dioksidi ya sulfuri.

Utafiti wa hivi karibuni uliofanwa Uingereza umegundua kwamba baadhi ya miti ina uwezo wa kupunguza chembechembe za uchafu hewani kwa hadi asilimia 79.

Miti inaweza kupunguza viwango vya mafadhaiko na kutusaidia kujisikia wenye furaha na afya njema. Chunguzi kadhaa zimeonyesha kwamba kutembea karibu na miti, au hata kutazama tu miti au maua kupitia dirishani, kunaweza kupunguza shinikizo la damu, kuongeza kinga ya mwili, kuboresha usingizi, kupunguza msongo wa mawazo na wasiwasi na hata kuharakisha mtu kupona baada ya kufanyiwa upasuaji.