NA ASIA MWALIM

SERIKALI ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema uimarishaji wa mitaala ya elimu nchini  unatokana na  haja ya kutaka mzunguko wa elimu kukamilika.

WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknelojia Profesa Joyce Ndalichako aliyasema hayo alipokua akifungua Mkutano wa Kupokea maoni ya Wadau wa elimu sekondari, huko Taasisi ya Chuo cha utalii Maruhubi.

Waziri Ndalichako alisema hatua hiyo ni kuendana na hali ya mabadiliko ya kijamii, kisiasa, kiuchumi, sayansi na teknelojia, pia kukidhi mahitaji ya Tanzania ya uchumi wa kati, viwanda na uchumi wa buluu.

Aidha alisema kuwepo mfumo  bora wa elimu nchini kutasiadia kukuza idadi  ya wanafunzi wabunifu na wenye uwezo mzuri wa kujiajiri na kuajiriwa, pia kuweka ushindani wa ajira katika soko la dunia.

Alisema Kutokana na nchi kujikita zaidi katika uchumi wa buluu na Viwanda, jambo ambalo huleta ushindani mkubwa wa soko la ajira ni nafasi pekee ya kutengeneza wahitimu bora watakaotokana na kupata taaluma za mapema kupitia mitaala itakayoweza kukidhi mahitaji ya sasa.

Akizungumzia kuhusu mabadiliko ya mitaala Profesa Ndalichako alisema tokea kupatikana uhuru wa Tanzania Serikali imefanya mabadiliko ya mitaala ya elimu mara tano, ambapo kila mtaala unaligana na mahitaji ya kielimu  yanayojitokeza kutokana na hali halisi.