HADI kufikia Agosti 31 mwaka huu Marekani itakuwa imeshaondosha wanajeshi wake wote nchini Afghanistan ambao wamedumu kwa takriban miongo miwili kupambana na makundi ya kigaidi ikiwemo Taliban na al Qaeda.

Marekani imepanga kubakisha kiasi cha wananchi 650 ambao watakuwa na jukumu maalum la kuulinda ubalozi wa nchi hiyo uliopo katika mji wa Kabul.

Wanajeshi wa Marekani wanaondoa chini humo ikiwa ni uamuzi wa rais wa nchi hiyo, Joe Biden ambaye hivi karibuni alikaririwa akisema kuwa ni wakati wa wananjeshi wa nchi yake kuondoka nchini Afghanistan baada ya kumalizika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Katika hali ya kushangaza kabisa jeshi la Marekani liliondoka uwanja wa ndege wa Bagram, ambacho ni kituo muhimu nchini Afghanistan usiku wa manane bila kuziarifu mamlaka za Afghanistan.

Kamanda mpya wa kituo hicho, jenerali Asadullah Kohistani alisema kwamba Marekani iliondoka Bagram majira ya saa 03:00 majira ya eneo hilo na kwamba jeshi la Afghanistan liligundua masaa kadhaa baadaye kuondoka kwao.

Bagram mbali ya kuwa kituo cha kijeshi kilichokuwa kikiendesha operesheni za anga, pia ina gereza linaloripotiwa kuwa na wafungwa 5,000 wa Taliban waliobaki katika kituo hicho.

Tangu vikosi vya Marekani vianz kufungasha virago nchini humo, kundi la Taliban limeanza operesheni huku wakiyachukua maeneo mengi na kuyaweka chini ya udhibiti wao.

Jenerali Kohistani alisema kwamba vikosi vya Afghanistan vinatarajia Taliban kumshambulia kambi ya Bagram na kwamba wamejiandaa kuvidhibiti dhidi ya mashambulizi hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye kituo hicho cha ndege, alisema tayari wameanza kupokea ripoti za kikundi hicho ambacho tayari kinajiimarisha kwa kufanya mashambulizi kwenye maeneo ya vijijini na kuelekea mijini.

“Unajua, ikiwa tunajilinganisha na Wamarekani, kuna tofauti kubwa,” Jenerali Kohistani alisema. “Lakini kulingana na uwezo wetu … tunajaribu kufanya bora na kadri iwezekanavyo kuleta usalama na kuwahudumia watu wote.”

Marekani ilitangaza kuwa imeondoka Bagram, ikimaliza vyema kampeni yake ya kijeshi nchini Afghanistan kabla ya tarehe rasmi ya kumalizika ya Septemba 11, iliyotangazwa na rais Joe Biden mapema mwaka huu.

Alipoulizwa na AP juu ya kujiondoa kwenye kituo hicho wakati wa usiku msemaji wa jeshi la Marekani, Kanali Sonny Leggett alirejelea taarifa iliyotolewa kwamba vikosi vya Marekani vilipanga kuondoka kwao kutoka kwa vituo kadhaa kwa kuwasiliana na kuwafahamisha viongozi wa Afghanistan.

Jenerali Kohistani ana askari karibu 3,000 chini ya amri yake wakilinganishwa na maelfu ya wanajeshi wa Marekani na washirika wake ambao waliwahi kuwa katika kambi hiyo ya kijeshi.

Bagram imedhibitiwa na vikosi mbali mbali kwa miaka mingi, ambapo kituo hicho kilijengwa na Wamarekani kwa Afghanistan katika miaka 1950 kabla ya kujikuta chini ya udhibiti wa Soviet wakati la Urusi lilipofanya uvamizi mwaka wa 1979

Baadaye ilichukuliwa na serikali ya Afghanistan iliyoungwa mkono na Moscow na kisha utawala wa mujahideen, kabla ya mwishowe kuchukuliwa na Taliban wakati kikundi hicho kilipoingia madarakani katikati ya miaka ya 1990.

Wakati Marekani ilipovamia Afghanistan mnamo 2001, iliondoa Taliban na kuchukua udhibiti wa uwanja huo wa ndege na kuubadilisha kuwa kituo kikubwa cha kupambana na Taliban.

Hivi karibuni wanajeshi wa Afghanistan zaidi ya 1,000 walikimbilia nchi jirani ya Tajikistan baada ya kukabiliana na wanamgambo wa Taliban, maofisa walisema.

Wanajeshi walikimbilia mpaka wa nchi hiyo jirani ili “kuokoa maisha yao wenyewe”, kulingana na taarifa ya walinzi wa mpaka wa Tajikistan.

Vurugu zimeongezeka nchini Afghanistan, na Taliban wamekuwa wakifanya mashambulizi na kuchukua maeneo zaidi katika wiki za hivi karibuni.

Kuongezeka kwa mashambulizi yao kumejiri wakati huu ambaokipindi cha miaka 20 ya huduma za jeshi la Nato kinafika tamati.

Idadi kubwa ya vikosi vya kigeni vilivyobaki nchini Afghanistan vimeondolewa kabla ya tarehe ya mwisho ya Septemba, na kuna wasiwasi kwamba jeshi la Afghanistan litaporomoka.

Chini ya makubaliano na Taliban, Marekani na washirika wake wa Nato walikubaliana kuondoa wanajeshi wote kwa ahadi ya wanamgambo kutoruhusu al-Qaeda au kikundi kingine chochote chenye msimamo mkali kuhudumu katika maeneo wanayodhibiti.

Kamati ya usalama ya Kitaifa ya Tajikistan, ambayo inasimamia usalama wa mpaka, ilisema kwamba wanajeshi wa Afghanistan walitafuta hifadhi mapema baada ya kupigana na wanamgambo wakati wa usiku, kulingana na shirika la habari la serikali la Tajikstan, Khovar.

Taliban sasa inadhibiti karibu theluthi moja ya Afghanistan, na inaendelea kukamata maeneo zaidi kila siku. Mikoa ya Badakhshan na Takhar, ambayo inapakana na Tajikistan, imeshuhudia harakati za hivi karibuni za Taliban kuteka maeneo makubwa

Hii ni mara ya tatu kwa wanajeshi wa Afghanistan kukimbilia Tajikistan katika siku tatu zilizopita na kisa cha tano katika wiki mbili zilizopita. Imefikisha jumla ya wanajeshi waliorejea Tajikistan kufika takriban 1,600.

Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani anasisitiza kuwa vikosi vya usalama vya nchi hiyo vina uwezo kamili kuwazuia waasi, hata hivyo kumekuwa na ripoti za wanajeshi zaidi wanaotafuta hifadhi nchini Pakistan na Uzbekistan kutoroka vita.

Nchi za jirani, pamoja na zile za Asia ya Kati, zinajiandaa kwa wakimbizi ikiwa vita vitaendelea nchini Afghanistan.

Vikosi vinavyoongozwa na Marekani viliondoa Taliban madarakani nchini Afghanistan mnamo Oktoba 2001. Kikundi hicho kilikuwa kikimpa hifadhi Osama Bin Laden na viongozi wengine wa al-Qaeda waliohusishwa na mashambulio ya 9/11 huko Marekani ambayo yalisababisha uvamizi huo.

Rais Biden amesema kujitoa kwa Wamarekani ni haki kwani vikosi vya nchi yake vimehakikisha Afghanistan haiwezi kuwa ngome ya wanajihadi wa kigeni kupanga njama dhidi ya nchi za Magharibi tena.