MOGADISHU, SOMALIA

MAREKANI imefanya shambulio la kwanza la anga dhidi ya wanamgambo wa Al-Shabab mjini Galkayo, kaskazini mwa nchi ya Somalia.

Inaelezwa kuwa hili ni shambulio la kwanza la angani tangu Rais wa Marekani Joe Biden kuingia madarakani.

Kwamujibu wa msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani Cindi Kingal amesema Marekani ilikuwa ikiyasaidia majeshi ya Somalia ambayo yalikuwa yakivamiwa na wanamgambo.

Hata hivyo zipo ripoti za awali zinazosema kuwa baadhi ya raia walijeruhiwa katika shambulio hilo lilolenga Al- Shabab.

Aidha hapo awali mtangulizi wake rais mstaafu wa Marekani Donald Trump aliwahi kufanya mashambulio ya angani nchini Somalia wakati wa utawala wake.

Somalia imekuwa ikikabiliwa na ukosefu wa usalama kutokana na mashambulio yanayofanywa na wanamgambo wa Al-Shabab.