WASHINGTON, MAREKANI

BUNGE la Marekani limepitisha sheria ya dharura itakayohakikisha usalama unaimarishwa kwenye jengo la bunge la Capitol Hill.

Hiyo imetokana na uvamizi wa jengo hilo uliofanyika Januari 6  na kuongezwa kwa idadi ya visa zitakazotolewa kwa watu walioshirikiana na Wamarekani katika vita vya Afghanistan.

Muswada huo wa dola bilioni 2.1 sasa utawasilishwa kwa Rais Joe Biden kutiwa saini.

Baraza la Seneti liliidhinisha sheria hiyo kwa kura 98-0, na mara baada ya hapo Baraza la Wawakilishi nalo likaupitisha kwa kura 416 na kupingwa kwa kura 11.

Muswada huo utaregeza vikwazo kadhaa vya visa, ambavyo wabunge wanasema ni muhimu katika wiki za mwisho ambapo wanajeshi wa Marekani wanaondoka nchini Afghanistan huku washirika wao wakiwaacha kwenye hatari ya kulipiziwa kisasi na wapiganaji wa kundi la Taliban.