WASHINGTON, MAREKANI

MAREKANI imetuma timu ya wataalam nchini Haiti kutathmini hali ya usalama na mahitaji mengine baada ya mauaji ya rais Jovenel Moise yaliotokea wiki iliyopita.

Aidha haikuwelezwa wazi taasisi zipi zimeshirikishwa, lakini timu hiyo inapanga kuwasilisha ripoti kwa rais Joe Biden itakaporudi nchini.

Inaelezwa kuwa hapo mwanzo, Marekani ilitupilia mbali ombi la Haiti la kuitaka kusaidia kuzima ghasia zilizofuatia kuuwawa kwa rais Moise siku ya Jumatano.

Kiongozi huyo ambaye aliuwawa kwa kupigwa risasi wakati akiwa nyumbani kwake, kwenye mji mkuu wa Port au Prince.

Idara ya polisi nchini humo imesema kuwa wamarekani wawili na wacolombia 26 baadhi yao wakiwa wanajeshi wa zamani, wamehusika kwenye shambulizi hilo, huku ikielezwa wengi wa washukiwa ambao ni raia wa Colombia bado wanaendelea kusakwa.

Hata hivyo ofisa mmoja kwenye utawala wa rais Biden amesema Marekani pia itashauriana na washirika wake wa kikanda pamoja na Umoja wa mataifa juu ya mzozo wa Haiti.