NA BENNY MWAIPAJA, DAR ES SALAAM

NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) itekeleze haraka maelekezo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuhusu Taasisi za Fedha kupunguza riba za mikopo.

Rais samia alitoa agizo hilo hivi karibuni ili kuwawezesha wafanyabiashara na Watanzania kwa ujumla kukopa na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.

Masauni alitoa maagizo hayo alipotembelea Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Benki hiyo ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake za kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango.

Alipongeza jitihada zinazofanywa na BoT kukutana na wadau ili kuhakikisha kuwa taasisi za fedha zikiwemo benki na watoa huduma wa sekta ndogo ya fedha wanapunguza riba za mikopo yao ili wananchi kupata mikopo yenye gharama nafuu.

“Niwapongeze kwa juhudi zilizoanza kuchukuliwa kuwezesha riba kupungua na ikiwezekana mwishoni mwa mwezi huu wananchi waanze kuona matokeo ya juhudi hizo kwa riba kuanza kupungua, kwa kuwa kupungua kwa riba ni jambo linalowezekana,” alieleza Mhandisi Masauni.

Aidha, aliitaka Benki hiyo kuhakikisha inaweka mikakati mahususi ya kuongeza akiba ya fedha za kigeni kwa kuwa na mbinu za kibunifu zikiwemo kuanza kununua na kuhifadhi dhahabu pamoja na kuongeza uuzaji wa bidhaa za Tanzania nje ya nchi na kusimamia kikamilifu shughuli za utalii.

Kuhusu suala la fedha za wananchi waliokuwa wateja wa benki ya FBME Limited iliyowekwa chini ya uangalizi wa Bima ya Amana za Wateja inayosimamiwa na Benki Kuu ikiwa katika hatua za kufilisiwa, Masauni, ameitaka benki hiyo kuhakikisha wateja wa benki hiyo wanarejeshewa fedha zao baada ya kukamilisha taratibu za kisheria zinazoendelea nchini Cyprus.

Kwa upande wake Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk. Bernard Kibesse, alimuhakikishia Naibu Waziri Masauni kwamba benki yake imeanza utekelezaji wa maagizo hayo kwa kuzungumza na mabenki ili washushe riba kama ilivyoelekezwa.

“Benki Kuu pia inaendelea kurekebisha kanuni mbali mbali za mikopo inayotolewa kwa mabenki ili kuziongezea ukwasi benki hizo ili na zenyewe zitumie fursa hiyo kushusha riba za mikopo,” alieleza Naibu Gavana.