Ashuka kusikiliza kero za wananchi, awataka kujiandaa

NA KHAMISUU ABDALLAH

MBUNGE wa Jimbo la Kikwajuni Hamad Yussuf Masauni, amewataka wananchi wa jimbo hilo kushirikiana pamoja katika mambo ya kimaendeleo ili jimbo lao liweze kupiga hatua.

Kauli hiyo, aliitoa wakati akizungumza na wananchi wa shehia mbalimbali za jimbo hilo ikiwemo Shehia ya Miembeni Jitini, Miembeni klabu na Michenzani wakati walipofika kwa ajili ya kusikiliza changamoto zinazowakabili na kutimiza ahadi zote walizozitoa katika kipindi cha kampeni.

Alisema wananchi hao wana umuhimu mkubwa kwani wamewapa kura kwa ajili ya kuwatumikia na wajibu wao kutekeleza ahadi zote walizoziahidi kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya jimbo lao ikiwemo huduma za maji safi na salama, elimu, huduma za afya na huduma nyengine muhimu.

Alisema ushirikiano wao ndio unaowapa ari zaidi ya kuhakikisha wanafanya mambo ya kimaendeleo ndani ya jimbo lao.

Aidha, alisema wamekuwa wakijitahidi sana katika kutatua changamoto za wananchi wa jimbo hilo ikiwemo kuwawezesha vijana kuweza kujiajiri wenyewe kwa kuwawekea kituo cha kujifunza cha TAI na kuwapatia mitaji.