NA ABOUD MAHMOUD

VIJANA nchini wametakiwa kutumia fursa za miradi inayotolewa na viongozi majimboni, ili waweze kufaidika nayo katika nyanja mbali mbali ikiwemo elimu.

Hayo yamesemwa na Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni Mhandisi, Hamad Masauni Yussuf, katika ukumbi wa elimu mbadala Rahaleo, wakati alipokua akikabidhi fedha kwa wanafunzi wa jimbo hilo wanaotarajia kujiunga na elimu ya juu katika vyuo vikuu mbali mbali .

Masauni ambae pia ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, alisema ubunifu wa miradi itawasaidia kupata kipato  na kuendesha maisha yao.

Hivyo, Mbunge huyo, aliwataka vijana hao kuendelea kusoma zaidi, ili kukamilisha malengo yao ikiwemo kuja kuitumikia nchi na vizazi vijavyo.

“Vijana nakuombeni kuzitumia fursa mnazozipata katika jimbo ambazo zinatokana na miradi mbali mbali inayoanzishwa na viongozi wenu kwa ajili ya kuwaletea maendeleo,”alisema.

Aidha, Masauni alisema Serikali imeanzisha mfuko wa elimu ya juu kwa Tanzania Bara na Visiwani, lakini kutokana na wanafunzi wanaopeleka maombi kuwa wengi hawawezi kutosheleza kupewa wote.

Hivyo ndio wakaamua yeye na viongozi wenzake wa Jimbo akiwemo Mwakilishi na Madiwani kuanzisha mfuko wa elimu wa jimbo ili kuwasaidia vijana ambao watakua hawana uwezo wa kuendelea na elimu hiyo.