NA JUMA SHAALI, JKU

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalumu za SMZ, Masoud Ali Mohammed, amepongeza jitihada zinazochukuliwa na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) kukamilisha mradi wa ujenzi wa skuli ya ufundi na sekondari, Mtoni. 

Pongezi hizo alizitoa wakati alipofanya ziara ya kutembelea kuangalia maendeleo ya utelekezaji wa mradi huo uliopo Mtoni, wilaya ya Magharibi ‘A’, Unguja.

Alisema ameridhishwa na jinsi ujenzi huo unavyoendelea na kusema kuwa ni jukumu la JKU kusimamia mradi huo kwa uadilifu ili kupata jengo imara kwa wakati.

Hata hivyo Massoud aliitaka JKU kufuata taratibu sahihi za manunuzi kwa kutafuta wazabuni wenye kuendana na matakwa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuepusha upotevu wa fedha unaojitokeza kwenye utekelezaji wa miradi kama hiyo.

“Naahidi kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili katika kutekeleza mradi huu ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku,” alisema Masoud.

Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Kujenga Uchumi, Kanali Makame Abdalla Daima, alimshukuru Waziri huyo kwa kutembelea mradi huo na kuahidi kuyafanyia kazi kwa vitendo maagizo na maelekezo yote yaliyotolewa.

Alieleza kuwa kufanya hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku lakini pia kuendana na kasi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Dk. Hussein Ali Mwinyi ambae ndiye Kamanda Mkuu wa Idara Maalumu za SMZ.

Vile vile Kanali Daima alimuomba Waziri Masoud kufanya ziara za mara kwa mara katika kuangalia miradi ya JKU ili kushajihisha kupatikana kwa ufanisi na morali wa wapiganaji katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akisoma taarifa ya ujenzi huo, Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Ufundi na Sekondari JKU Mtoni, Kanali Jabir Saleh Simba, alisema kukamilika kwa mradi huo kutatoa fursa kwa vijana zaidi ya 1,500 kupata elimu ya ufundi na ujasiriamali ili kukabiliana na changamoto ya ajira.