NA MADINA ISSA

WAZIRI wa Nchi, Afisi ya Rais, Tawala za Mikoa serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed, amewataka watendaji wa Ofisi hiyo wakiwemo Madiwani, kuendelea kufanyakazi kwa ushirikiano kuanzia ngazi ya Shehia, Wadi, Wilaya, Mkoa na Wizara ili lengo liweze kufikiwa.

Aliyasema hayo, alipokuwa akizungumza na Madiwani wa Mkoa wa Mjini Magharibi, ofisini kwake Vuga,  kilichowashirikisha Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, Mkoa wa mjini Magharibi na wakuu wa Wilaya hiyo, Mamea pamoja na Makaimu Wakurugenzi wa Wilaya zilizopo katika Mkoa huo.

Hatua hiyo inafanyika ikiwa ni mikakati ya kuona utendaji wa kazi katika Wizara hiyo unakwenda kama ulivyopangwa pamoja na kumtambulisha Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu walioapishwa hivi karibuni.

Alisema serikali hairidhishwi na kutokuwepo kwa ushirikiano katika taasisi za kiserikali, jambo ambalo linawarejesha nyuma upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi.

Alisema ni vyema viongozi wa Wilaya wanapotoa matamko ya mikoa yao kuwajulisha viongozi wao wanaowasimamia, ili kuweza kutia baraka zao za kiutendaji.

“Tusiposema sasa hivi baadae tutapata shida hivyo ni vyema watendaji tuwe na ushirikiano wa pamoja katika kazi zetu” alisema.