NCHI kadhaa za Afrika zipo katika migogoro ya mipaka na kutishia usalama pamoja na kutia hatarini uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo.
Ukoloni ulipomalizika baada ya nchi nyingi kujipatia uhuru kuna mataifa ambayo hayakusuluhisha migogoro ya ni nani anayemiliki nini hasa katika sehemu za mipakani.
Hivi karibuni nchi nyingi za Afrika zimejikuta katika malumbano hayo, lakini mzozo kati ya Kenya na Somalia kuhusu anayemiliki sehemu ya bahari hindi ndio unaogonga vichwa vya habari kwani kesi hiyo sasa ipo kataika mahakama ya kimataifa baada ya nchi hizo mbili kukosa kupata suluhisho la nje ya korti.
Tanzania na Malawi zinatofautiana kuhusu aliye na haki ya kumiliki Ziwa linalozitenganisha nchi hizo mbili. Nchini Tanzania ziwa hilo linaitwa ziwa nyasa lakini kwa Malawi ziwa hilo ni ziwa Malawi.
Kwa miongo kadhaa mataifa yote mawili yanadai kumiliki ziwa hilo na hata wakati mmoja Malawi ilitishia kuishtaki Tanzania katika mahakama ya kimataifa ya haki huko Hague.
Mzozo huo ni mojawapo ya malumbano ya mipaka ambayo nchi za Afrika zilirithi kutoka enzi za ukoloni kwani Malawi inasema mpaka wa ziwa hilo unafaa kutegemea mkataba wa mwaka wa Anglo-German wa mwaka wa 1886.
Malawi inasema msimamo wake kuhusu mpaka halisi pia unatagemea azimio la Cairo la mwaka wa 1964 ambao uliamuru kwamba mipaka yote ya mataifa itasalia kama ilivyorithiwa kutoka kwa viongozi wa ukoloni kabla ya nchi hizo kupata uhuru.
Tanzania kwa upande wake imetofautiana na tafsiri hiyo ya Malawi ikisema sheria inayofaa kutegemewa ni ile kwamba kila taifa linamiliki nusu ya ziwa hilo na mpaka upo katikati ya ziwa lenyewe.
Mifano ya maziwa ambayo yanimilikiwa nusu kwa nusu ni kama ziwa la Geneva linalomilikiwa kwa pamoja na Ufaransa na Switzerland, ziwa Chad katika mipaka ya Chad, Cameroon, Niger na Nigeria
Kenya na Somalia: Kinachozozaniwa ni nini? Kwa miaka kadhaa Kenya na Somalia zimekuwa zikitofautiana kuhusu mpaka wa majini katika bahari hindi.
Mahakama ya kimataifa ya haki inatarajiwa kuanza kusikiza kesi hiyo mwezi Machi -uamuzi ambao utaifurahisha nchi moja na kuihamakisha nyingine. Nchi hizo zinazozania eneo la umbo la upembe lenye ukubwa wa kilo mita 100,000 mraba katika bahari hindi.
Kenya inasema mpaka huo unapaswa kufuata mstari wa moja kwa moja unaoipa sehemu kubwa ya bahari hindi na tayari Kenya imeshatoa leseni za uchimbaji mafuta kwa kampuni kadhaa katika eneo linalozozaniwa.
Somalia kwa upande wake inataka mpaka huo kubadilishwa ili kuipa umiliki wa sehemu inayozozaniwa. Uamuzi wa kesi hiyo huenda ukaamua jinsi nchi hizo mbili zitakavyohusiana kidiplomasia katika siku zijazo.
Mataifa ya Kenya na Uganda yamewahi kuzozania kisiwa kidogo katika Ziwa Victoria kwa jina Migingo. Raia wengi wa Kenya wanalalamika kuhusu kunyanyaswa na maofisa wa polisi na jeshi wa Uganda na baadaye ikaibuka kwamba Uganda ilikuwa ikidai kukimiliki kisiwa hicho.
Nchi hizo mbili hata hivyo ziliunda jopo la pamoja ili kuamua mmiliki halisi wa kisiwa hicho hatua iliyopunguza wasi wasi wa mzozo kutokea na kuvuruga uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Wakenya wengi wakati huo waliilaumu serikali ya rais mstaafu Mwai Kibaki kwa kutochukua hatua za kuwalinda wakenya waliokuwa wakihangaishwa na maofisa wa usalama wa Uganda. Kwa sasa kuna utulivu katika kisiwa hicho na wafanyibashara wa nchi zote mbili wanaendesha shughuli zao katika kisiwa cha Migingo
Ethiopia na Sudan: Mnamo katikati ya mwezi Februari mwaka wa 2021 Sudan ilimuita balozi wake nchini Ethiopia baada ya nchi hizo mbili kufufua mzozo wa mpaka wa eneo al-Fashqa baada ya kila nchi kudai kumiliki sehemu kubwa yenye rutuba na iliyokuwa ikitumiwa na wakulima kutoka Ethiopia.
Kila nchi iliilaumu nyingine kwa kutekeleza mauaji katika sehemu hiyo huku wanajeshi kadhaa wakiripotiwa kuuawa katika mzozo huo. Sudan imeishtumu Ethiopia kwa kukatalia ardhi yake na kuwatuma wapiganaji katika eneo hilo ambao wamedaiwa kuwashambulia wanajeshi wa Sudan.
Hata hivyo, Ethiopia imedai kwamba kuna ‘mtu wa tatu’ anayeichochea Sudan kuzua mzozo katika eneo hilo la mpakani na kuhataraisha usalama wa nchi hizo mbili na hasa wakati huu ambapo serikali ya Addis Ababa inakabiliana na viongozi wa Tigray ambao imewataja kama magaidi.
Mzozo huo wa Ethiopia na Sudan umezua hofu ya uwezekano mkubwa wa vita kati ya nchi hizo mbili jambo ambalo linaweza kuhatarisha kabisa usalama katika kanda hii na upembe wa Afrika.
Sudan Kusini na Sudan: Sudan na Sudan Kusini zimekuwa zikilumbana kuhusu anayemiliki jimbo la Abyei katika mpaka wa nchi hizo mbili.
Mzozo huo uliibuka baada ya Sudan Kusini kujinyakulia uhuru kutoka kwa Sudan mwaka wa 2011. Wakaazi wa jimbo hilo walijaribu kufanya kura ya maoni ili kujiunga na Sudan Kusini lakini uamuzi huo ulitiwa doa na Sudan Kusini.
Eritrea na Ethiopia: Eritrea na Ethiopia zimekuwa katika mzozo wa mpakani kwa muda mrefu zikipigania eneo la wa Badme. Nchi hizo zimewahi kupigana kwa zaidi ya miaka 10 na baadaye Eritrea kujitenga na kuwa nchi huru.