NA ABOUD MAHMOUD
JAMII imetakiwa kuwa wawazi wanapofikwa na matatizo ya aina mbali mbali ambayo yanayosabisha kuleta msongo wa mawazo ili kupatiwa ushauri nasaha.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, Wanawake na Watoto, Nassor Ahmed Mazrui, alipokua akizindua kitabu cha ‘My little yellow book’ chenye maudhui ya afya ya akili katika ukumbi wa hoteli ya Serena Inn, mjini Unguja.
Mazrui alisema msongo wa mawazo ni chanzo kikuu kinachowafanya watu kukosa ufanisi wa majukumu na kuzorotesha maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla.
“Natoa wito kwa wananchi wote wa Zanzibar na kwengineko duniani, mtu yoyote ambae anajiona ana msongo wa mawazo au wasiwasi asifiche awaeleze watu walio karibu nae ili wamsaidie maarifa kwani akifanya hivyo atapunguza matatizo aliyonayo na atapata unafuu”, alisema.
Alisema katika jamii kumekuwa na matukio mbali mbali ikiwemo kupigwa kwa watoto, mke au mume lakini matukio kama hayo huchukuliwa ni ya kawaida ambapo huwa ni ugonjwa.
Pia alisema Zanzibar kumekuwa na tatizo ambalo linaikabili jamii la ubakaji na udhalilishaji ambapo alisema matukio hayo yanatokana na mfanyaji kuwa na tatizo la afya ya akili.
Hivyo alisema ni wajibu wa jamii kukubaliana na hali hiyo wakati anapojihisi hayupo sawa na kuieleza jamii inayomzunguka ili aweze kupewa ushauri nasaha kwa ajili ya afya yake.
Sambamba na hayo Mazrui alisema mazingira ya Zanzibar yanaweza kumfanya mtu aweze kupona maradhi mbali mbali ya afya ya akili akitolea mfano wa mtunzi wa kitabu hicho.
“Mtunzi wa kitabu hichi ambae alipokuja Zanzibar akiwa na tatizo hilo, alipona na kurudi hali yake na kupata maarifa ya kutunga kitabu hicho,” alieleza.
Naye Mkurugenzi wa Fikraafya, Shabir Khalfan alisema dunia inapoteza dola Milioni 2.5 trilioni katika biashara na uwekezaji kutokana na kuwepo kwa tatizo hilo.
Hivyo alisema jamii inatakiwa kuweka mkakati wa kupambana na unyanyapaa kuhusiana na afya ya akili hasa katika mawazo chanya kwani alisema jamii ina matatizo makubwa.
Shabir alitoa takwimu kwamba kila sekunde arubaini mtu mmoja hupoteza maisha ambapo alisema asilimia kubwa ni vijana ambapo asilimia 90 wana matatizo ya afya ya akili.
“Ni wazi kwamba tupambane na tatizo la afya ya akili na kijamii tuwakubali hawa wanaopitiwa na tatizo hilo kwa kuwasaidia kwani tusipowasadia tutapoteza vijana wetu wengi, na sasa hivi unyanyapaa umezidi,” alisema.