NA KHAMISUU ABDALLAH

JESHI la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, linamshikilia Rahima Juma Khamis (42) mkaazi wa Bububu Kigamboni kwa tuhuma za kurekodi ushahidi na kupiga picha kwa kutumia simu yake ya mkononi katika mahakama ya Mkoa Vuga.

Rahima ambaye ni mwalimu wa skuli ya chekechea Arif ya Tomondo Mshelishelini, alidaiwa kuingilia mahakama kutaka kuharibu ushahidi dhidi ya kesi tatu zinazomkabili mshitakiwa Shamir Kombo Ali.

Akizungumza na Zanzibar Leo kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Awadh Juma Haji, alisema mtuhumiwa huyo alitenda tukio hilo Juni 30 mwaka huu majira ya saa 3:00 asubuhi katika mahakama ya Mkoa Vuga katika chumba cha waendesha mashitaka.

Alisema mtuhumiwa huyo alipatikana katika chumba hicho akionekana akipiga picha na kurikodi kwa kutumia simu yake ya mkononi ushahidi wa kesi tatu za makosa ya udhalilishaji zinazomkabili mshitakiwa Shamir ambae anashitakiwa katika mahakama hiyo.

Aidha alisema mshitakiwa huyo anatuhumiwa kuwafanyia vitendo vya kuwadhalilisha kubaka, kuingilia kinyume na maumbile na shambulio la aibu wasichana watatu.

“Kabla ya kesi kuanza mahakamani ni lazima waendesha mashitaka wafanye maandalizi na mashahidi wao au kujiandaa wao wenyewe kwa yale watakayozungumza mahakamani, wakati wakiwa na mashahidi wao mama huyu alitoa simu yake na kuanza kupiga picha na kurikodi,” alisema.

Aidha Kamanda Awadh, alibainisha kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa akiwalaghai walalamikaji wahanga wa matukio hayo kwa kuwataka kuharibu ushahidi kwa lengo la kumsaidia mshitakiwa wa kesi hizo.

Hata hivyo, alisema katika uchunguzi unaoendelea imebainika kuwa mtuhumiwa Rahima ana uhusiano na mshitakiwa huyo kwani nae ni mwalimu. “Hawa watu wawili wanafahamiana kwa sababu mtuhumiwa ni mwalimu na mshitakiwa inaonesha anakwenda kusomesha huko,” alisema.

Alisisitiza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi dhidi ya mtuhumiwa huyo na pale utakapokamilika basi atafikishwa mahakamani.

Kamanda Awadh, alitoa onyo kali kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya kuharibu ushahidi wa kesi mbalimbali hasa za makosa ya udhalilishaji kwa kuwalaghai walalamikaji kwa lengo la kutaka kuwasaidia watuhumiwa wa makosa hayo kuacha mara moja kufanya hivyo.

Alisema serikali inapiga vita mambo hayo hivyo aliwasisitiza kuacha tabia hiyo na badala yake ni jukumu lao kutoa ushirikiano kwa serikali dhidi ya vita hivyo na vita nyengine ili kukomesha vitendo hivyo.

“Vita hivi sio vya serikali pekee au vyombo vinavyosimamia sheria bali ni vita vya pamoja kati ya serikali, vyombo vya sheria na wananchi kwa ujumla kwani bila ya ushirikiano wa wananchi basi vitendo vya udhalilishaji litakuwa gumu kumalizika nchini,” alisisitiza.

Kamanda Awadh alisema wananchi wana wajibu mkubwa wa kushiriki na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola na vyombo vyengine vya sheria ili kuona wafanyaji wa matukio hayo na matukio mengine wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.