NA HAFSA GOLO
MWAKILISHI wa Jimbo la Donge Dk. Khalid Salum Mohamed, amewataka vijana kuitumia michezo na tamaduni zao kwa kuwa zina mchango mkubwa katika ustawi wa jamii na upatikanaji wa ajira.
Dk. Khalid alieleza hayo wakati akizungumza na wanamichezo wa jimbo la Donge katika kikao maalumu cha kuimarisha na kuibua vipaji vipya vya wanamichezo jimboni humo .
Alisema iwapo vijana hao watatumia vyema tamaduni na mila zao itasaidia kuimarika sekta ya utalii sambamba na wao kuwekeza katika ajira mbadala.
Alisema wakati serikali inaendelea na mipango imara ya kuimarisha utalii na uchumi wa buluu, ni vyema nao vijana wakahakikisha wanajipanga kudumisha mila, desturi na utamaduni wa asili kwani ni miongoni mwa vivutio kwa wageni wengi wanaoingia nchini.
“Ipo michezo na ngoma mbali mbali za asili, jambo la msingi ni kujikubalisha kuikuza na kuendeleza utamaduni wenu tena lazima mfahamu kwamba tamaduni ni hazina muhimu inayohitajika kulindwa,” alisema.
Aidha aliwataka vijana hao kujenga utamaduni wa kusoma historia ya nchi yao jambo ambalo litawajengea ari na uzalendo wenye kwenda pamoja na uchapakazi na ubunifu.
Alisema michezo mbali ya kuwa chanzo cha ajira, pia huimarisha umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa wananchi hivyo wawe tayari kufuata maelekezo ya viongozi wao.
“Michezo inawafanya vijana kutumia muda wenu vizuri badala ya kukaa vijiweni na kufanya vitendo visivyokubalika na hatimae kupoteza utu wenu,” alisema.
Sambamba na hilo, aliahidi kuviboresha viwanja vya michezo jimboni humo ili viweze kukidhi viwango vya kitaifa pamoja na kuvipatia vitendea kazi vikundi vyote vya tamaduni na mazoezi jimboni humo kwa kushirikiana na viongozi wa jimbo hilo.
Nae Mbunge wa Jimbo hilo, Soud Mohamed alisema viongozi wa jimbo hilo wamejipanga kutumia eneo la michezo iwe ni sehemu ya vijana na wanawake waweze kujiajiri wenyewe.
Hivyo aliwasihi kuhakikisha wanatekeleza kazi zao kwa ufanisi sambamba na kuongeza juhudi na kuweka kipaumbele cha malengo walioyakusudia.
Kwa upande wake Nahodha Msaidizi wa timu ya Mtelezo, Haji Mchezo alisifu juhudi za viongozi hao katika kuimarisha michezo jimboni humo pamoja na kuwapatia vifaa na mahitaji mengine ya kimichezo anapopata fursa.
“Ukaribu na hamasa zako zinatuongeza ari na ufanisi wa kucheza soka sambamba na kuweka malengo ya kuongeza utaalamu ili tuweze kushirikia mashindanio mbali mbali ndani na nje ya Zanzibar,” alisema.
Nae Jamila Juma alisema wataendelea kudumisha masuala ya michezo na tamaduni huku akiwaomba viongozi hao kuendeleza utamaduni wa kubadilishana mawazo na vijana wa jimbo hilo kwa maslahi ya jimbo.