BERLIN, UJERUMANI

KANSELA wa Ujerumani, Angela Merkel ameelekea Marekani kama sehemu ya ziara zake za kuaga kabla ya kuondoka madarakani.

Merkel anatarajiwa kukutana na Rais Joe Biden ambapo watazungumzia masuala kadhaa ikiwemo kuimarisha uhusiano kati ya Ujerumani na Marekani, janga la virusi vya corona, na mradi wa bomba la gesi unaogharamiwa na Urusi na Ujerumani.

Aidha inaelezwa kuwa Merkel atakutana na Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris na maafisa wengine wa ngazi ya juu wa nchi hiyo.

Inaelezwa kuwa baada ya kufanya kazi na Merkel kwa miaka 16, maafisa wengi wa Marekani na kwengineko duniani hawaelewi Ujerumani itachukua hatua gani baada ya uchaguzi wa kansela Septemba 26.

Wakati akiwa madarakani, Merkel amefanya kazi na marais wanne wa Marekani, wakati huo huo, Chama cha Waandishi wa Habari nchini Ujerumani, DJV kimemsihi Merkel kumshawishi Biden aondoe mashtaka yanayomkabili mwanzilishi wa tovuti ya Wikileaks, Julian Assange.