PARIS, Ufaransa
NI mchezaji mpole na makali yake yamefahamika kudhihirika pindi anapojitosa uwanjani.Ni miongoni mwa wachezaji wanaotambulika kote dunia na isitoshe amesalia katika klabu moja tangu alipoanza kucheza, Barcelona .
Jina lake ni Lionel Andres Messi au Leo Messi, na alizaliwa Juni 24 mwaka wa 1987. Ni nahodha wa timu ya taifa ya Argentina na anazingatiwa kuwa mojawapo ya wachezaji bora wa nyakati zote . Messi ameshinda tuzo za Ballon d’Or mara sita .
Katika muda wake wote wa maisha yake ya soka na klabu ya Barcelona, Messi, ameshinda makombe 34 yakiwemo 10 ya La liga , Ciopa Del Rey saba na Kombe la Uefa mara nne.
Messi anashikilia rekodi za kufunga magoli mengi katika La Liga (474).
Amefunga zaidi ya mabao 750 katika mechi za klabu na nchi ndiye mchezaji aliyeifungia klabu mabao mengi zaidi .
MWANZO WA SAFARI
Alizaliwa na kukulia kati kati mwa Argentina, Messi alihamia Hispania na kujiunga na Barcelona akiwa na umri wa miaka 13, na kuichezea klabu hiyo kwa mara ya kwanza Oktoba 17 mwaka wa 2004.
Alijiimarisha kama mchezaji muhimu wa klabu ndani ya miaka mitatu iliyofuata, na katika msimu wake wa kwanza bila ya kukatizwa mnamo 2008-09 aliisaidia Barcelona kufanikiwa kushinda mataji matatu ya soka nchini humo na akiwa na umri wa miaka 22, Messi alishinda tuzo yake ya kwanza ya ‘Ballon d’Or’.
Misimu mitatu ya mafanikio ilifuata, na Messi kushinda ‘Ballons d’Or’ nne mfululizo, na kumfanya kuwa mchezaji wa kwanza kushinda tuzo hiyo mara nne mfululizo. Wakati wa msimu wa 2011-12, aliweka rekodi za La Liga na Ulaya kwa magoli mengi yaliyofungwa katika msimu mmoja, huku akijitambulisha kama mfungaji bora wa wakati wote wa Barcelona.
Misimu miwili iliyofuata, Messi alimaliza wa pili kwa tuzo ya ‘Ballon d’Or’ nyuma ya Cristiano Ronaldo (mpinzani wake katika taaluma), kabla ya kupata hali yake bora kimchezo katika kampeni ya 2014-15 na kuwa mfungaji bora wa muda wote La Liga na kuongoza Barcelona kushinda mataji matatu kwa mara ya pili, baada ya hapo alipewa tuzo ya tano ya ‘Ballon d’Or’ mnamo 2015.Messi alishika unahodha wa Barcelona mnamo 2018, na mnamo 2019 alishinda tuzo ya sita ya ‘Ballon d’Or’.
MAISHA YA FAMILIA
Tangu 2008, Messi amekuwa katika mahusiano na Antonela Roccuzzo, mzaliwa mwenzake wa Rosario. Anamfahamu Roccuzzo tangu akiwa na umri wa miaka mitano, kwani yeye ni binamu wa rafiki yake wa karibu tangu utotoni, Lucas Scaglia, ambaye pia ni mchezaji wa soka.
Baada ya kuweka uhusiano wao siri kwa mwaka, Messi alithibitisha mapenzi yao kwanza kwenye mahojiano mnamo Januari 2009, kabla ya kujitokeza hadharani mwezi mmoja baadaye wakati wa sherehe huko Sitges baada ya ‘dabi’ ya Barcelona-Espanyol.
Messi na Roccuzzo wana watoto watatu: Thiago (aliyezaliwa 2012), Mateo (aliyezaliwa 2015) na Ciro (aliyezaliwa 2018).
Ili kusherehekea ujauzito wa kwanza wa mpenzi wake, Messi aliweka mpira chini ya shati lake baada ya kufunga katika ushindi wa 4-0 wa Argentina dhidi ya Ecuador mnamo Juni 2 2012, kabla ya kuthibitisha ujauzito huo katika mahojiano wiki mbili baadaye.
Thiago alizaliwa Barcelona mnamo Novemba 2, 2012, na Messi akihudhuria kuzaliwa baada ya kupewa ruhusa na Barcelona kukosa mazoezi.Alitangaza kuwasili kwa mtoto wake kwenye ukurasa wake wa Facebook, akiandika, “Leo mimi ndiye mtu mwenye furaha zaidi ulimwenguni, mtoto wangu alizaliwa na shukrani kwa Mungu kwa zawadi hii!”
Alikosa mazoezi kabla ya mechi dhidi ya Atlético Madrid kuhudhuria kuzaliwa kwa mtoto wake wa pili, Mateo, mnamo Septemba 11, 2015 huko Barcelona. Mnamo Juni 30, 2017, alimuoa Roccuzzo katika hoteli ya kifahari iitwayo Hotel City Center huko Rosario na wageni wapatao 260 walihudhuria harusi yake.Mnamo Oktoba 15, 2017, mkewe alitangaza wanatarajia mtoto wao wa tatu katika ujumbe wa Instagram, na maneno “Familia ya 5”.
Mnamo 10 Machi 2018, Messi alikosa mechi dhidi ya Málaga baada ya Ciro kuzaliwa.
Messi ana uhusiano wa karibu na watu wa familia yake, hasa mama yake, Celia, ambaye amechora uso wake kwenye bega lake la kushoto.
Mambo yake ya kitaalamu yanaendeshwa sana kama biashara ya familia: baba yake, Jorge, amekuwa wakala wake tangu akiwa na miaka 14, na kaka yake mkubwa, Rodrigo, anashughulikia ratiba yake ya kila siku . Mama yake na kaka yake mwengine, Matias, wanasimamia shirika lake la hisani, Leo Messi Foundation, na hushughulikia maswala ya kibinafsi na ya kitaalamu huko Rosario
TUHUMA ZA KUKWEPA KULIPA KODI
Mambo ya kifedha ya Messi yalichunguzwa mnamo 2013 kwa tuhuma za ukwepaji kodi. Kampuni za katika nchi za Uruguay na Belize zilitumika kukwepa euro milioni 4.1 kwa ushuru unaohusiana na mapato ya udhamini kati ya 2007 na 2009.
Kampuni moja huko Panama iliyoanzishwa mnamo 2012 ilitambuliwa baadaye kuwa ni ya familia ya Messi katika uvujaji wa data ya Panama Papers.
Messi, ambaye alidai kutofahamu mpango huo, alilipa kwa hiari malimbikizo ya milioni 5.1 mnamo Agosti 2013.
Mnamo Julai 6, 2016, Messi na baba yake walipatikana na hatia ya udanganyifu wa ushuru na walipewa adhabu ya kifungo cha miezi 21 jela na na waliamrishwa kulipa euro milioni 1.7 euro milioni 1.4 mtawalia kama faini .
Akiwa mbele ya hakimu, alisema, ” Mimi hucheza soka tu.Nilitia saini mikataba kwa sababu nilimwamini baba yangu na mawakili na tuliamua kwamba watasimamia shughuli hizo’
MAFANIKIO YA HIVI KARIBUNI
Lionel Messi alimaliza kusubiri taji kuu la kwanza la kimataifa wakati Argentina ilipoifunga Brazil kwenye fainali ya Copa America kwenye uwanja wa Rio wa Maracana kwa goli 1-0 mnamo Julai 13.
Messi (34), alianguka chini kwa furaha wakati kipenga cha mwisho kilipopulizwa na alikimbiiwa kwa haraka na wachezaji wenzake, kabla ya kurushwa hewani kwa sherehe, kwani mwishowe alipata heshima ya kiwango cha juu na nchi yake katika mashindano ya 10 muhimu kwake .
Alisaidia pia kumaliza kipindi cha miaka 28 cha Argentina tangu waliposhinda mashindano hayo na aliteuliwa kuwa mchezaji wa mashindano baada ya mabao yake manne kwenye kipute kizima .
Imekuwa miaka 15 tangu Messi awakilishe Argentina kwa mara ya kwanza kwenye mashindano makubwa na baada ya mashindano manne ya Kombe la Dunia na mechi sita za Copa America, akicheza mechi 53, mwishowe ana taji kuu la kimataifa yeye na nchi yake, imetamani kuafikia hilo.
Licha ya kuwa mmoja wa wachezaji bora sana na mahiri wa enzi ya kisasa na wakati wote na mataji 10 ya La Liga, manne ya ligi ya Mabingwa na Ballons d’Or sita, masuali juu ya ukosefu wake kung’ara kimataifa yametanda juu yake urithi wake.
Kushindwa mara kwa mara na Argentina limekuwa jambo chungu kwa mshambuliaji huyo, ambaye aliwahi kutangaza kustaafu kwake, kabla ya baadaye kutengua uamuzi huo baada ya kupoteza fainali ya pili mfululizo ya Copa America mnamo 2016, kushindwa kwake kwa mara ya tatu katika fainali ya mashindano hayo na miaka miwili tu miaka baada ya kushindwa katika fainali ya Kombe la Dunia ya 2014.
Bado kuna matarajio ya Messi kwenda kutumia fursa yake labda ya mwisho kushinda Kombe la Dunia – jambo ambalo Argentina hawajafanya tangu 1986 – ikiwa ataiongoza nchi yake kwenda Qatar akiwa na umri wa miaka 35 mnamo Disemba 2022.