NA MWANAJUMA ABDI, DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaban amesema mfumo wa utoaji wa taarifa za biashara kimataifa wa kidigitali utaleta mapinduzi na mageuzi katika sekta ya biashara na viwanda.

Hayo aliyasema jana, wakati akizindua mfumo wa Biashara, uliozinduliwa kwa mara ya kwanza Tanzania, ambapo ni nchi ya nne kwa Afrika Mashariki kutumika, uliofanyika katika Viwanja vya Maonyesho ya 45 ya Biashara ya kimataifa SabaSaba jijini Dar es Salaam.

Alisema mfumo huo utaondosha ukiritimba wa uombaji kibali, leseni na usajili wa kuagiza bidhaa na kuuza ndani na nje ya nchi, ambapo mfumo kama huo unatumika nchini Kenya, Rwanda na Uganda.

Alisema mfumo huo utasaidia kufanya mageuzi makubwa ya biashara kwa kupatikana taarifa sahihi katika eneo moja kupitia mfumo wa kidigitali, ili kuondosha urasimu uliokuwepo huko nyuma.

Alieleza moja ya changamoto na kilio kikubwa cha wafanyabiashara ni upatikanaji wa taarifa sahihi za biashara, hivyo uzinduzi wa mfumo huo umekuja na majibu ya changamoto zilizokuwa zinawakabili wafanyabiashara nchini.

Alisema kutakuwa na dirisha moja la kupata taarifa za kufanya biashara, ambapo taasisi zote zimeshirikishwa kikamilifu na sekta ya umma na sekta binafsi ili kuondosha sintofahamu kwa wafanyabiashara.

Alifafanua kuwa, taarifa zimeunganishwa za ndani na nje ya nchi kwa kuweka wazi juu ya upatikanaji wa vibali, leseni na usajili za kuweza kufanya biashara kwa kuuza na kununua bidhaa nje na ndani ya nchi.

Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Shaaban Said Omary na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kagahe wakibonyeza kitufu kuashilia uzinduzi Mfumo wa Taarifa za Biashara kwa njia ya Mtandao (Trade Portal) uliofanyika viwanja katika Maonesho ya 45 ya Biashara Kimataifa yanayoendelea Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Sabasaba jijini Dar es Salaam.

Naye Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe alisema mfumo huo una faida za kutekeleza mpango wa tatu wa maendeleo wa kimataifa, ambao unasisitiza kuwa na uchumi shindani kwa maendeleo ya watu.

Alisema biashara na shughuli mbali mbali zitafanyika kwa utaratibu rahisi wa mfumo wa kidigitali kwa kuondosha urasimu usiokuwa wa lazima, ambao unasababisha ukiritimba wa kwenda kujaza fomu na kutolewa sababu nyingi zisizo za msingi kwa wafanyabiashara.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tan Trade), Balozi Mteule Edwin Rutageruka alitaka watanzania wabadilike na kamwe wasibaki nyuma hivyo waende kidigitali katika kukuza uchumi kupitia sekta ya biashara.