NA KHAMISUU ABDALLAH

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesema itaweka mfumo mmoja wa taarifa katika bandari ya Zanzibar ili taasisi zilizopo bandari zifanye kazi zao kwa ufanisi.

Mfumo huo unalenga kuimarisha utendaji wa taasisi zinazofanya kazi katika bandatri hiyo kutekeleza wajibu wao katika kuwahudumia wafanyabiashara kwa urahisi zaidi.

Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Jamal Kassim Ali, alieleza hayo wakati wa ziara aliyoifanya katika bandari hiyo kwa lengo la kujionea hali halisi ya utendaji kazi ndani ya bandari hiyo hasa suala la ushushaji na upakiaji wa makontena.

Alisema bado kuna changamoto ya upashanaji taarifa zinazotoka katika mamlaka moja kwenda nyengine kutokana nakutokuwepo mifumo inayosomana hivyo taarifa kupelekwa kwa njia za karatasi hali inayosababisha wafanyabiashara kuchelewa kupata mizigo yao na kutokana na urasimu.

Alisema katika kipindi cha wiki moja, wanatarajia kuwaita wataalamu waliopo nchini ambao wametengeneza mifumo mingi ukiwemo ZAN Malipo na mifumo ya ZRB ili kutengeneza mfumo huo utakaoleta ufasini katika shirika hilo.

“Lazima tutengeneze mfumo unaokwenda na wakati, utakaooana mambo yote yanafanyika kwenye kompyuta hatutaki tena mambo ya makaratasi sasa tupo katika dunia ya sayansi na teknologia kwenye makatasi yanatuchelewesha,” alisisitiza.

Mbali na hayo, Jamal alipongeza jitihada zinazochukuliwa na shirika hilo kuipatia ufumbuzi tatizo la mrundikano wa makontena ambalo kwa sasa limepungua kwa kiasi kikubwa na kuwaomba kuendelea kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi ili makontena yasichukue muda mrefu kukaa bandarini.

Aidha alisema lengo la serikali ni kuhakikisha bandari ya Zanzibar inafanya kazi kwa ubora na ufanisi mkubwa ambao utapelekea mizigo mingi kuja Zanzibar na kusafirishwa kupitia bandari ya Zanzibar.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Huduma za Bandari na Uendeshaji wa Shirika hilo, Injinia Mansour Rashid, alisema hivi sasa changamoto ya uchelewaji wa utoaji wa makontena katika bandari hiyo haipo tena kwani hivi sasa wanajitahidi kufanya kazi masaa 24 ili kuona msongamano huo unaondoka bandarini.