NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAM

KLABU ya Simba ya jijini dar es salam imemzawadia Kocha Mkuu wa timu ya wanawake ya klabu hiyo Mussa Hassan ‘Mgosi’ kwa kuiongoza timu yake hiyo kutwaa ubingwa wa ligi kuu soka la wanawake kwa mara ya pili mfululizo.

Mgosi ambae aliiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa huo kwa mara ya pili mfululizo,  baada ya kupokea zawadi hiyo aliwashukuru viongozi na wachezaji wa klabu hiyo kwa kufanikisha ushindi huo.

“Asante Simba Sports Club kwa zawadi ya gari ila makabidhiano naomba yawe siku ile ya mechi ya Simba SC wakikabidhiwa kombe la VPL hii itasaidia kwa wachezaji kuiga maadili ya kuitumikia Simba kwa nidhamu na uadilifu,” alieleza Mgosi kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Kocha huyo aliongeza kuwa, ‘Nichukue fursa hii kuwashukuru TFF (shirikisho la soka Tanzania), benchi la Twiga Stars na uongozi wa Simba kwa kufanikisha Simba Queens kupata mechi ya kujipima na kuiangalia nini kifanyike kabla ya michuano ya kimataifa kuanza matokeo ni kitu kingine”.

Mgosi aliongeza kuwa anaamini kwa ukanda wa CECAFA ngazi ya vilabu hakuna timu bora yenye wachezaji bora kama timu ya taifa hivyo aliomba wachezaji hao kupatiwa nafasi za kucheza ili kuijenga timu hiyo la kitaifa.