Malengo, ndoto za wananchi zaopotea

MIAKA 10 iliyopita ama muongo mmoja tunaizungumzia Julai 9 ya mwaka 2011 Afrika ilishuhudiwa kuzaliwa nchi mpya ya Sudan Kusini, ambapo taifa hilo limejitenga kutoka Sudan.

Ilikuwa furaha kubwa kwa wapenda amani na maendeleo wote barani Afrika na jumuiya ya kimataifa, lakini ilikuwa furaha kubwa kwa wananchi wa Sudan Kusini waliokuwa na matumaini makubwa kwa kuzaliwa taifa lao jipya.

Wananchi wa Sudan Kusini walikuwa na kila sababu ya kuwa na matumaini na maisha mapya baada ya nchi yao kupata uhuru hasa ikizingatiwa kuwa walipotia kwenye wakati mgumu kutokana na mapigani yasiyokwisha.

Ndo za Wasudani Kusini ziliwaminisha kupatikana kwa uhuru bila shaka kutafanikisha kuponya majeraha ya vita, migogoro na machafuko na kupatikana kwa amani ya kudumu itakayofungua ukurasa mpya wa amani, usalama na maendeleo.

Mambo ya uendeshaji wa nchi yalianza vyema na wananchi wa taifa hilo waliamini waliyokuwa wakifikiria ikiwemo kuwa na amani, kuepuka migogoro, machafuko na kupiga hatua kubwa za kimaendeleo itawezakana.

Lakini miaka mitatu baada ya taifa hilo kujipatia uhuru wake, matumaini yote ya wananchi wa Sudan Kusini yalipotea kama waliotema mate kwenye mto wenye kutiririsha maji.

Kilichoshuhudiwa ni vikosi vya jeshi la Sudani Kusini vilianza kushambuliana baada ya tofauti za kisiasa baina ya rais wa nchi hiyo Salva Kiir na Riek Machar ambao wote walikuwa wakitoka chama kimoja SPLM.

Mapigano yalianzia katika mji mkuu Juba baada ya rais wa nchi hiyo, kumtuhumu makamu wake Riek Machar pamoja na viongozi wengine 10 kuwa na njama za kutaka kuipindua serikali yake.

Machar akakimbia na kuelekea mafichoni na kuongoza uasi kupitia kundi la SPLM/IO, huo ukawa mwanzo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe katika taifa hilo changa zaidi barani Afrika ambavyo viliendelea kwa miaka sita na kusababisha maelfu ya watu kupoteza maisha.

Vita hivyo viliwavunja moyo watu wengi ambao walikuwa wanalipigia upatu taifa hilo kushika njia ya maendeleo na kujikwamua kutoka lindi la umasikini wa wananchi wake.

Hata hivyo, kwa wafuatiliaji wa siasa na harakati za chama cha SPLM huo ulikuwa ni mwendelezo tu wa siasa za mapambano baina ya makamanda wa kundi hilo.

SPLM iliundwa mwaka 1983 na John Garang na wafuasi wake ambao walikuwa ni wanajeshi walioasi kutoka vikosi vya nchi ya Sudani na mnamo mwaka 2013 chama hicho kilitimiza miaka 30 kwa mapambano mapya baina ya Kiir na Machar.

Lakini hata kuzaliwa kwa SPLM kwenyewe kunahusishwa na mapambano ya kutokuelewana kwa makamanda wakuu.

Wakati Garang na wafuasi wake wakiasi kutoka katika safu za jeshi la utawala wa Khartoum, walikutana na wapiganaji wa kundi la Anyanya II ambao walikuwa ni mwamvuli wa makabila zaidi ya 60 ya kusini mwa nchi hiyo ambao walikuwa hawautambui utawala wa Sudan.

Awali makundi hayo mawili yaliungana kwa kuwa yalikuwa na lengo moja, lakini muda mfupi tu baadae mgogoro mkubwa ukatokea juu ya uongozi wa harakati zao na kusababisha vita vilivyochukua miaka mitatu.

Katika vita hivyo, uongozi wa Anyanya II ulipigwa na kundi la Garang na hatimaye wapiganajji wote wa kusini kuwa chini ya amri yake.

Riek Machar kabla ya kukosana na Kiir baada ya uhuru inasemekana kuwa alikwishawahi kuwa na uhasama na Garang kabla ya uhuru kutokana na utofauti wa mitazamo.

Garang alikuwa akiamini kupigania usawa na kuthaminiwa kwa watu wa kusini ndani ya nchi ya Sudan, lakini Machar alitaka mapambano yajikite katika kutafuta uhuru wa kuunda taifa la jipya la watu wa kusini.

Kutofautiana kwa mtazamo baina ya wawili hao kulimsukuma Machar kujiondoa SPLM mwaka 1991 na kukabiliana na vikosi vya Garang mpaka walipokubaliana kuweka tofauti zao na Machar kurejea SPLM miaka 11 baadae mnamo mwaka 2002.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya wafuasi wa Kiir na Machar japo vilianza kwa kutofautiana kisiasa, lakini ilitumbukia katika tofauti za kikabila na kufanya athari zake kuwa mbaya zaidi.

Kiir anatokea katika kabila kubwa zaidi nchini humo la dinka wakati Machar akitokea kabila la Nuer ambalo ni la pili kwa ukubwa.

Vita hivyo pia vilifumua kidonda chengine cha zamani cha nchi hiyo ambacho ni matumizi ya ya watoto kama wapiganaji ambapo mashirika ya misaada ya kimataifa yanakisia kuwa zaidi ya watoto 17,000 waliingizwa kwenye mapigano.

Miaka sita ya vita hivyo vilivyosita mwezi Februari mwaka 2020 imeshuhudiwa zaidi ya watu 400,000 kupoteza maisha na zaidi ya watu milioni nne wameyakimbia makazi yao, kati ya hao watu milioni 1.8 wakiwa wakimbizi wa ndani na zaidi ya watu milioni 2.5 wakikimbilia nchi jirani.

Vita hivyo pia vimesababisha janga la umasikini nchini humo ambapo watu wanaishi maisha duni huku mfumko wa bei ukishuhudiwa ukipanda mpaka asilimia 300.

Katika miaka sita ya mapigano wananchi walikumbwa na mabaa ya njaa, kutokana na mapambano yalikita mizizi kwenye maeneo ambayo yanategemewa kwa kilimo hali ambayo iliwazuia raia kutolima kwa ufanisi ama kuyakimbia makaazi yao kabisa.

Majanga mengine ya njaa yalikuwa ni ya kutengeneza, serikali ya Marekani pamoja na mashirika ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu yaliituhumu serikali ya Kiir kuzuia misaada ya chakula kutofika katika maeneo ambayo waasi wanaungwa mkono.

Katika miaka sita ya vita hivyo, juhudi kadhaa za kikanda zikiongozwa na mataifa ya IGAD, EAC pamoja na nchi jirani kama Kenya, Ethiopia, Uganda, Sudan na hata Tanzania na Afrika Kusini zilifanyika ili kusitisha mapambano hayo.

Makubaliano kadhaa yalifikiwa ya kusitisha mapigano lakini hayakufua dafu. Makubaliano ya kwanza kabisa yakifanyika Januari ya 2014 lakini hayakuheshimiwa na mapambano yakaendelea.

Septemba mwaka 2018 Kiir na Machar waliingia makubaliano lakini makubaliano hayo ya kusitisha mapambano ya miaka mitano kwa wakati yalichukua muda kufanikishwa na yalikutana na vigingi kadhaa ikiwemo mgawanyo wa madaraka pamoja na kuwajumuisha makundi mengine madogo ya waasi katika serikali ya pamoja.

Mwezi Aprili mwaka 2019, viongozi hao wawili walikutana na Papa Francis huko Vatican na katika hali iliyostaajabisha wengi Papa aliwapigia magoti wote wawili na kubusu miguu yao kama ishara ya kuwaomba wasirejee katika mapigano.

Hatimaye Februari mwaka 2020 Machar alirejea serikalini kwa kuapishwa tena kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na kumaliza kabisa mgogoro huo mbaya zaidi wa kisiasa na kibinaadamu nchini humo.