-
Hekima na busara ndivyo vinavyomsaidia katika kazi yake vyenginevyo asingedumu
-
Aliwahi kubambikiwa kesi ya kushirikiana na timu kwa ushirikina
-
Ataka vyumba vya wachezaji Amaan vitengenezwe viwe vya kisasa.
Na Mwajuma Juma
Juma Makungu Simai (58), anasimulia kazi yake ya kufunga na kufungua Uwanja wa Amaan kila siku kukiwa na mechi au hakuna ikiambatana na visa na mikasa.
Anasema mwanzoni hakuwa anajua kama kazi hiyo ya kufunga na kufungua milango ya Uwanja wa Amaan ni kazi ambayo inakuwa na utaratibu wake.
Anaeleza kuwa wakati anaaza kuingia katika uwanja huo alikuwa anamuona mtu tu akifanya shughuli yake hiyo na kuchukulia ni jambo la kawaida.
Anasema kwa takriban miaka 10 alikuwa akifika katika uwanja huo, lakini hakuweza kutambua lolote linalohusiana na kazi hiyo ilikuwa ikifanywa na marehemu Mfaume Mwinyi, aliyefariki mwaka 2013.
Akizungumza na gazeti hili Simai ambae ni mzaliwai wa Dunga Bweni , Wilaya ya Kati Unguja, anasema mbali na kufanya majukumu mengine uwanjani hapo lakini kazi yake kubwa ni kutunza vyumba vya wachezaji.
Anasema kuwa kabla ya kuanza na jukumu hilo aliajiriwa ndani ya uwanja huo kama tarishi na baadae akahamishiwa katika bustani na sasa kazi yake ni kushughulikia bustani na kutunza vyumba hivyo vya wachezaji.
Simai anasema alinaza kazi ya kufunga kufua uwanja wa Amaan mnamo mwaka 2015 baada ya Mfaume Mwinyi kufariki na ikawa hakuna mtu mwengine.
“ Kazi hiyo ya kufunga na kufungua milango niliianza mwaka 2015 baada ya aliyekuwepo Mfaume Mwinyi kufariki dunia”, alifahamisha.
Alieleza kuwa anaipenda kazi yake hiyo , kwani ndio maisha yake ingawa anakabiliana na changamoto ambazo anasema ni sehemu ya maisha .
“Changamoto nnazopitia kwangu nazichukulia ni za kawaida, wachezaji ni kama watoto wanaharibu vitu, ambapo kwangu naichukulia kuwa ni jambo la kawaida”, alisema.
Alieleza kuwa tokea kuanza kazi hiyo kitu ambacho hatokisahau katika maisha yake, ni baada ya kuambiwa kuwa alimruhusu mchezaji kuingia katika chumba cha timu pinzani kufanya ushirikina jambo ambalo halikuwa kweli.
Alisema tukio hilo lilimsikitisha sana kutokana na kwamba kesi yake ilifikishwa mpaka kwa wakuu wake wa kazi.
“Nakumbuka ilikuwa mwaka jana (2020) siku ya mchezo kati ya Zimamoto na KVZ, nilivumishiwa kwamba Zimamoto waliingia katika chumba cha KVZ, wakati haikuwa kweli na siku hii sitoisahau katika maisha yangu maana kesi ilikuwa kubwa”, alisema.
Hata hivyo, anasema kuwa pamoja na watu wengi kudhania kuwa mara nyingi mshughulikiaji wa uwanja hasa vyumba vya wachezaji, anatumiwa kuweka vitu vya kishirikina siku ya mchezo au kabla, lakini yeye hajawahi kufanya hivyo.
“Sijawahi wala sitowahi maana najua madhara yake, kwani hapo nyuma alikuwepo mzee mmoja ambae ameshafariki alifanya hivyo na alipooza miguu”,alisema.
Alifahamisha kwamba vitendo hivyo vinakuwa vinafanyika hasa kwa wenyewe viongozi wa timu na mara nyingi huvifanya siku ile ile ya mchezo, lakini sio kwa majira ya usiku.
Alisema kuwa wakati mwengine huja labda saa moja kabla ya mchezo au masaa mawili, lakini inakuwa ni siku ya mchezo ambao inakuwa yeye anachukulia kuwa ni muda wake wa kuanza kazi yake.
“Vinafanyika na wala sikutanii kwa hili, lakini wapo wanaokuja kufanya kwa siri na wengine kwa dhahiri ambao hata wewe mwenyewe ukiwa ni mdau mkubwa wa kuingia uwanjani hapa unayaona”, alisema.
Simai aliongeza kwa kusema “Ni kweli watu huja wakafanya vitendo vya kishirikina na hata baada ya mechi utakuta vitu chumbani kama herizi, vikaratasi vilivyoandikwa maandishi ya Kiarabu na makombe yaliyotapakaa”.
Akizungumza kwa kujiamini na kuonesha kuijali kazi hiyo,mfanyakazi huyo alifahamisha kwamba wakati mwengine anapokuta vitu kama hivyo huwaita wenyewe na kuwataka waviondoshe na yeye baadae kufanya kazi yake ya usafi.
Hata hivyo, alisema kuwa pamoja na kuwa vitendo hivyo vinafanyika, lakini hajawahi kutoa taarifa kwa yoyote.
“ Hii ni kwa sababu matendo ambayo yanafanyika sio siri maana mengine yanakuwa yanafanyika uwanjani mbele ya hadhara ya watu, ingawa mengine yanafanyika kwa siri”, alibainisha.
“Wengine wanajua ni utani kumuona mtu anamwaga maji, lakini wakati mwengine inakuwa kuna ukweli ndani yake”,aliongeza.
Alisema mara nyingi vitendo ambavyo hufanyika utakuta mara timu haiingii vyumbani mpaka atoke mtu mmoja kwanza au wengine hufikia uwanjani moja kwa moja.
Aidha, alisema timu nyingi zina imani sana na ushirikina kiasi kwamba nyengine hukataa kupitia mlango wa kuingilia wachezaji.
“Kwa hapa kwetu hakuna timu ambazo hazirogi, lakini wengine hawafanyii hapa uwanjani bali huja kumalizia tu na wengine wanazidiana, lakini siwezi kuzitaja kwa majina”, alisema.
Alifahamisha kwamba masula hayo yanafanyika kila kukicha, lakini yeye huacha na kuendelea na kazi yake kwa kuwa mambo hayo huona yeye kama yeye hayamuhusu.
“Kuna matukio hufanywa kwa siri na mengine kwa dhahiri, maana wakati mwengine nimo ndani utasikia kitu kinapigwa ukitoka humuoni mtu au hata kama ukimuona humjui”, alisema.
Changamoto nyengine anayopitia ni ya kikazi zaidi ambapo watu hutaka kupita zaidi ya idadi ambayo wanatakiwa na anapowakatalia huonekana mbaya.
“ Kwa utaratibu timu inatakaiwa kupita na watu 37, lakini wakati mwengine huja mpaka na watu 40 au zaidi, jambo ambalo hunipa wakati mgumu”, alifahamisha Simai akionesha kukerwa na ubabe wanaotumia viongozi wa timu.
Hata hivyo, Simai anasema kuwa mafanikio ambayo anayapata ni kupata ushirikiano mzuri na wafanyakazi wenzake pamoja na kupata umaarufu mkubwa kwa viongozi na wachezaji ambao wengi wao humfanya kama babu yao.
Simai ambae anatarajia kustaafu mwakani (2022),anasema kuwa pamoja na kuwa ni kazi rahisi, lakini sio hivyo kwa sababu kuna utaratibu wake ambao kama muangalizi unatakiwa kuufata.
“Mwanzoni nilikuwa naiona kazi nyepesi, lakini kumbe sivyo ila kwa sasa nimeizoea na ndio naendelea nayo”, alisema.
Hata hivyo, kwa upande wa ushabiki anasema kuwa yeye ni mpenzi na mshabiki mkubwa wa timu ya Simba na kwa Ulaya Manchesta United na kwa Zanzibar hana timu ambayo anaishabikia kutokana na mzingira yake anayofanyia kazi.
“Siwezi kuwa na timu hapa na hata kama nnayo, lakini imo ndani ya moyo wangu kwa sababu nikiweka dhahiri kutokana na mzingira ya kazi yangu watu watakuwa na mashaka na mimi siku itakapokuwa inacheza. Kwa hivyo, nimeamua kuwa kimya na timu za hapa”, alisema.
Sambamba na hayo Simai anaiomba Wizara ya Habari kuviangalia upya vyumba vya wachezaji kwa kuvifanyia matengenezo kutokana na kuchakaa na kuwa katika hali ya kisasa.
Anasema katika vyumba hivyo kunahitaji matengenezo ili viweze kwenda sambamba na vigezo vya kimataifa.
“Zamani katika vyumba hivyo kulikuwa na mabenchi ya kukalia waalimu, lakini sasa hayapo na badala yake wakati wa mechi za kimataifa hulazimika kuweka viti”, alibainisha.
Hata hivyo, anasema kwa kuwa viongozi ambao wameteuliwa kushika nyadhifa ndani ya wizara hiyo baadhi yao wanalijua hilo, ni imani yake kwamba watalifanyia kazi.
Simai akitoa ushauri wake atakapostaafu ansema mtumishi wa umma ambae atapata nafasi hiyo ashirikiane vyema na wachezaji pamoja na viongozi, ili aweze kwenda nao sambamba.
“Hii sehemu ni ngumu na mtu ambae anawekwa hapa asiwe mkali, atumie busara na hekma hasa kwa mechi za ndani ambapo idadi ya kuingia watu inakuwa inapitiliza kwa kutaka kuingia wengi badala ya 37 ambao ndio kwa mujibu wa kanuni na sheria”, alisema.
Juma Makungu Sima ana mke mmoja na watoto wanne wakiwemo wawili wanawake na wawili wanaume.