NI miaka 70 imetimia tangu kusainiwa kwa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kuwalinda wakimbizi, ambapo licha ya mkataba huo kuwepo kwa miongo saba sasa, wataalamu wanasema bado hakuna nia ya dhati ya kisiasa ya kulinda haki za wakimbizi waliotawanyika maeneo mbalimbali ulimwenguni.

Mkataba wa kuwalinda wakimbizi wa Geneva ni wa msingi katika kuwalinda wakimbizi, ambapo unaelezea na kutoa ufafanuzi wa kina mkimbizini mtu wa namna gani na haki zake ni zipi na wajibu walio nao.

Watu walioondoka nchini mwao kutokana na hofu ya kuteswa kwa sababu ya mbalimbali ikiwemo rangi zao, dini, utaifa, uanachama wao katika kundi fulani la kijamii ama kutokana na misimamo yao ya kisiasa, kama ilivyoainishwa kwenye maandishi ya mkataba huo, wana haki ya kuwa kwenye kundi hilo.

Kutokana na vita ya pili ya dunia na kukua kwa mivutano, Umoja wa Mataifa ulipitisha makubaliano hayo mjini Geneva mnamo mwaka mwaka 1951, ambapo mwanzoni baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, ulijikita kuwalinda baadhi ya watu pekee hasa wakimbizi wa Ulaya.

Ili kutenda haki kutokana na mabadiliko ya hali halisi duniani kote, makubaliano yalitanuliwa mnamo mwaka 1967 na nchi 149 zimetia sahihi moja ya mikataba au yote miwili.

UNHCR imekuwa ndio mlinzi au mhifadhi wa mkataba huu tangu mwanzo hadi sasa na inaendelea kuhakikisha kuna hifadhi ya kimataifa kwa watu waliofurushwa kutoka nyumbani kwao.

Mchambuzi kutoka taasisi ya sera za uhamiaji wa mjini Brussels, Susan Fratzke alisema hata sasa, mkataba huo una jukumu muhimu kwani ndiyo waraka pekee unaozitaka nchi ziwalinde wakimbizi.

Suzan anasema hivi sasa watu wanalazimika kuhama makaazi yao kwa sababu mbalimbali kuliko katika wakati ambapo dunia ilikiwa kwenye vita baridi.

“Mkataba huu haujitekelezi wenyewe, hii inamaanisha kuwa serikali zinazotia sahihi zinapaswa kuzitimiza ahadi zao wanazozitoa kwenye mkataba huo katika sheria za nchi zao.

Na nchi nyingi hufanya hivi kupitia sheria ya kuomba hifadhi inayoonesha ni nani inamtambua kama mkimbizi na ni haki zipi alizonazo kwa kuzingatia makubaliano ya mkataba,” alisema Fratzke.

Naye Abiy Ashenafi, mkuu wa ofisi ya uhamiaji katika kituo cha haki za binadamu cha chuo kikuu cha Pretoria nchini Afrika ya Kusini alisema anafikiri kuwa Umoja wa nchi za Afrika haujaelezea baadhi ya mapungufu kwenye maana hasa ya neno mkimbizi.

Alisema tatizo kwenye mkataba huo ni kuwa hautoi utaratibu wa malalamiko kwa wakimbizi dhidi ya nchi zinazowapokea.

Kulinda haki za binadamu ni jambo analolipenda Hamado Dipama aliyewahi kuwa mkimbizi. Amejitolea kufanya hivyo tangu alipokimbia machafuko ya kisiasa nchini mwake Burkina Faso.

Takribani miaka 20 iliyopita wakati akiwa bado mwanafunzi yeye na wengine wengi walipinga udikteta wa rais Blaise Compaore aliyeitawala nchi hiyo kwa mkono wa chuma kwa miaka 27 hadi pale alipopinduliwa kupitia maandamano ya mwaka 2014. Alijikuta akiishia katika mji wa Munich wa jimbo la Bavaria, Ujerumani ambako sasa anapaita nyumbani.

“Wakati nilipokuwa nakimbia machafuko, sikujua kuhusu makubaliano ya wakimbizi ya Geneva. Hili sio suala la nchi masikini, watu kule wana taarifa kidogo kuhusu hili. Hilo ni pengo. Ni pale tu nilipofika Ujerumani ndipo nilipoanza kukumbana nalo.

Kwa sababu kwa wakati ule nilikataliwa. Ni kwa nini watu wengine walindwe lakini si mimi? Ingawa nilikuwa naweza kueleza kuhusu hali yangu Burkina Faso, kuwa niliteswa nikiwa mwanafunzi katika vuguvugu dhidi ya dikteta Blaise Compaoré, hiyo yote haikusaidia.”

Mara nyingi anaona suala la kurudishwa nyumbani kwa lazima kuwa si sahihi. Kwa mfano wakati watu walioishi Ujerumani muda mrefu na kisha wanarudishwa kwenye nchi zao ambazo bado hazijawa imara.

Dipama anafahamu hofu ya kurejeshwa nyumbani. Aliishi kama mkimbizi kwa miaka tisa na alipambana na hilo. Alipata hati ya ukaazi mnamo mwaka 2014.

Mwezi mmoja uliopita alituma maombi ya kupatiwa uraia anasema haikuwa rahisi kwa sababu anapaswa kuirudisha paspoti yake ya Burkina Faso.

Tangu mwaka 2017 amekuwa msemaji wa baraza la wakimbizi la Bavaria na ameanzisha kikundi cha watu wenye asili ya Afrika kinachopigania maslahi ya watu weusi.

Anasema mataifa yanapaswa kufanya yalichotia sahihi kwenye mkataba wa kuwalinda wakimbizi na kufanya marekebisho ili wakimbizi wapate ulinzi zaidi kutoka kwenye mataifa yenye matatizo.

Kwa hakika baada ya miaka 70, mkataba huu bado una umuhimu kuliko wakati wowote ule, kwani unatoa muongozo kwa nchi juu ya ulinzi wa wakimbizi, na unatoa wito wa ushirikiano wa kimataifa na kusaidia wakimbzi.

Kwa kuzingatia idadi kubwa ya watu wanaovuka mipaka, mito, majangwa na baharí ili kusaka usalama, ni muhimu sana nchi zote zikatia saini mkataba huo.

Mkataba huu unaweza kuonekana ni maandishi tu lakini kwa wakimbizi umebeba mambo mazuri. Unaruhusu sote kuota ndoto ambayo siku moja wale waliolazimika kukibia wanaweza kupata pahali wanaita nyumbani.