NA MWANDISHI WETU, MOROGORO

 MKAAZI wa Kinole, wilaya ya Morogoro vijijini, Abdallah Mohammed (50), ameshinda promosheni ya ‘Bonge la Mpango’ na kukabidhiwa zawadi ya gari yenye thamani ya shilingi millioni 169.

Promosheni hiyo iliyokuwa ikiendeshwa na benki ya NMB, ilimalizika rasmi Jumatano wiki hii ambapo Mohammed alikabidhiwa gari hiyo Toyota Fortuner katika hafla ya makabidhiano yaliyofanjika katika soko kuu la chifu Kingalu karibu na tawi la NMB la Wami mjini Morogoro juzi.

Akizungumza kabla ya kukabidhi zawadi hiyo, Kaimu Ofisa Mkuu wa Ukaguzi wa Ndani wa benki hiyo, Benedicto Baragomwa, alisema promosheni hiyo ililenga kubadilisha maisha ya watanzania ambapo zawadi mbali mbali zilikabidhiwa kwa wateja 120 walioshinda katika promosheni hiyo.

Baragomwa alieleza kuwa mbali ya gari na fedha taslimu, zawadi nyingine zilizokabidhiwa ni pikipiki za magurudumu matatu aina ya LIFAN na gari ndogo aina ya TATA Ace.

“NMB ilifanya uwekezaji huu kwa kutambua mchango wa wateja wake katika mafanikio yake ikiwa ni pamoja na kuandika historia katika tasnia ya kibenki kwa kupata faida kubwa,” alieleza Baragomwa.

Aliongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2020, benki hiyo ilitengeneza faida ya shilingi bilioni 206, hivyo promosheni hiyo pia ililenga kurudisha faida hiyo katika maendeleo ya wateja wake.

Naye Meneja wa Tawi la Mt. Uluguru, Lilian Abraham, alieleza kufurahishwa kwake na mshindi ya promosheni hiyo kutokea mkoani humo na mshindi kuwa mwanakijiji jambo linaloonesha kuwa wananchi wote wameanza kuona umuhimu wa kuweka fedha zao benki.

Akizungumzia ushindi wake, Mohammed alieleza kuwa haikuwa rahisi kuamini kwamba ameshinda licha ya kuwa na matumaini hayo toka promosheni hiyo ilipozinduliwa.

Aliongeza kuwa pamoja na gari hilo kulitumia katika shughuli zake za usafiri na familia yake, amejipanga kujiendeleza zaidi katika kilimo na biashara huku akiwaomba wananchi wenzake kutumia huduma za benki hiyo ili kujihakikishia fursa mbali mbali ikiwemo ya zawadi kama hizo.